TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kukamilisha uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu 1,385 kati ya 1,387 wanaotakiwa kisheria.
Taarifa hiyo imetolewa mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Tume, Ramadhani Kailima, ambaye amesema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa masharti ya sheria zinazohusu mamlaka za wilaya, mamlaka za miji na Sheria ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 2024.
Kailima amesema uteuzi huo umezingatia matakwa ya kisheria yanayolenga kuhakikisha uwakilishi wa wanawake katika uongozi wa serikali za mitaa. Ameeleza kuwa idadi ya walioteuliwa inaendana na uwiano wa kura na matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa yaliyofanyika mwaka huu.
Hata hivyo, nafasi mbili zilizobaki za Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu zitasubiri kukamilika kwa uchaguzi wa marudio katika kata za Mindu na Chamwino (Manispaa ya Morogoro) pamoja na Mzinga (Manispaa ya Temeke), ambako uchaguzi uliahirishwa kufuatia vifo vya baadhi ya wagombea.
Katika mgawanyo wa viti hivyo, vyama vitano vimepata nafasi za Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu. Vyama hivyo ni CCM, ACT-Wazalendo, CHAUMMA, CUF na NCCR-Mageuzi, kwa mujibu wa asilimia ya kura walizopata katika uchaguzi uliopita. SOMA : Mjumbe INEC ataka uadilifu uchaguzi mkuu
Tume imesema imewasilisha orodha ya majina ya walioteuliwa kwa Makatibu wa Vyama husika kwa ajili ya hatua nyingine za kiutendaji. Aidha, imeahidi kuendelea kusimamia taratibu zote hadi kukamilika kwa uteuzi wa madiwani wawili waliobaki mara tu uchaguzi wa marudio utakapoafikiwa.
