MKUU wa Wilaya ya Uyui, Mohammed Mtulyakwamu, ameongoza dua maalum ya kuliombea Taifa kwa ajili ya kustawisha amani ya nchi na maendeleo endelevu.
Akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo, Mtulyakwamu amesema kuwa mafanikio ya taifa yanategemea umoja, mshikamano na utulivu wa wananchi. Aliongeza kuwa dua kama hizo zitaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya, ikiwemo Tarafa ya Igalula na Tarafa ya Uyui, ambapo matukio makubwa ya kijamii yatarajiwa kuandaliwa. . SOMA: Amani ni msingi wa taifa, tudumishe amani
Aidha, amewakumbusha wananchi kudumisha amani ambayo Tanzania inaendelea kufurahia, akibainisha kuwa mataifa mengi yanaitamani lakini si rahisi kuipata. Alisisitiza kuwa umoja wa Watanzania na kudumisha mila na desturi njema ni msingi mkubwa wa kuzuia migogoro na vitendo vya vurugu.
Dua hiyo imeelezwa kuwa ni mwanzo wa mfululizo wa mikusanyiko ya kiimani itakayojumuisha watu kutoka makundi mbalimbali katika jamii, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za maendeleo na utulivu nchini.
