BAADA ya Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah, kuiongoza timu hiyo katika mechi nne za Ligi Kuu Bara msimu huu bila kuonja ladha ya ushindi, amesema ana kazi kubwa ya ziada ya kufanya kwa kikosi hicho, ili kiondokane na mwenendo mbaya uliopo.
Josiah aliyejiunga na Dodoma Oktoba 16, 2025 baada ya kocha raia wa Rwanda, Vincent Mashami, kutokidhi vigezo vya kusimamia benchi, amekiongoza kikosi hicho katika mechi nne, ambapo kati ya hizo amepoteza tatu huku akitoka sare mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema matokeo yanayotokea uwanjani ni ngumu kuamini kutokana wachezaji wa timu hiyo kufuata vyema maelekezo yake, ingawa jukumu lake kama kocha ni kuendelea kuwajenga kisaikolojia na wala sio vinginevyo.
“Kimbinu kwa aina ya uchezaji tunaotaka kuutumia wachezaji wanafuata na kutekeleza maelekezo yangu vizuri, ingawa kwangu ukiniuliza mwenendo huu nitakwambia ni kukosa bahati na sio kama wapinzani wetu wanatuzidi sana,” amesema Josiah.
Josiah aliyewika na timu za Tunduru Korosho, Biashara United ‘Wanajeshi wa Mpakani’, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons, amesema kama kocha kuna muda unapitia presha kutokana na hali hiyo, ingawa wachezaji waliopo wanampa matumaini.
“Kiwango cha utimamu wa mwili kwa wachezaji ni kweli kuna muda kinakuwa chini na kusababisha kuchelewa kufanya uamuzi katika baadhi ya maeneo uwanjani na kuwapa faida wapinzani wetu ya kutuadhibu, ila kuna mabadiliko yameanza kuonekana.”