
LICHA ya ugumu wa Ligi Kuu ya Wanawake Hispania lakini mshambuliaji wa Kitanzania, Opah Clement ameendelea kupata nafasi kwenye kikosi cha SD Eibar.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars alitambulishwa kikosini hapo akitokea FC Juarez ya Mexico aliyoitumikia kwa msimu mmoja akicheza mechi sita kati bila ya kufunga bao wala asisti.
Tangu ametambulishwa kikosini hapo, Opah alicheza mechi nane kati ya 11 ilizocheza timu hiyo iliyopo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kati ya mechi hizo nane alicheza dakika 493 akifunga bao moja Septemba 28 dhidi ya Levante bao lililoipa Eibar pointi tatu muhimu.
Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Granada akimaliza dakika zote 90, Oktoba 04 alicheza dakika 75 dhidi ya Barcelona, Costa Adeje (68), Real Sociedad (64), Dep La Coruna (30), Athletic Bilbao (67) na Espanyol akicheza dakika 11.
Kasi, nguvu ni miongoni mwa vitu vinavyomfanya Opah aendelee kuaminiwa na kupewa nafasi kwenye kikosi hicho kilichosheheni nyota kutoka mataifa mbalimbali duniani.