
BEKI wa kushoto wa Azam FC ya vijana, Ismaili Omari amesaini mkataba wa miezi sita kuitumikia klabu ya AIK Solna inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden.
Agosti mwaka huu Azam FC ilitangaza wachezaji watatu Omari na viungo washambuliaji wawili Mohamed Shillah na Adinan Rashid kutoka timu ya vijana waliopelekwa klabuni hapo kwa majaribio.
Taarifa iliyoipata Mwanaspoti ni mmoja wa nyota huyo Omari tayari amesaini mkataba wa miezi sita baada ya kufaulu majaribio ya awali huku wengine wawili wakiangalia hatua za mwisho.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeliambia gazeti hili kuwa beki huyo kama ataendelea kuonyesha kiwango kizuri ataongezewa mkataba wa miaka mitatu.
“Tayari amesaini mkataba wa miezi sita, wanaendelea kujiridhisha na kiwango chake na ataongezewa miaka mitatu mingine lakini hadi sasa anaonyesha matumaini makubwa na huenda msimu ukianza akasaini,” kilisema chanzo hiko na kuongeza
“Wale wengine wawili bado wanaendelea kuangaliwa kwa ukaribu lakini kuna uwezekano mkubwa na wao wakachukuliwa tunasubiri ligi irejee tujue hatma yao.”
Kwa takwimu zao Shillah kwenye mechi tatu amefunga mabao manne, Adinani mechi mbili mabao mawili huku Omari alicheza mechi tatu na kutoa asisti mbili.
Chama hilo limemaliza nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi ya Sweden kwenye mechi 30 imeshinda 13, sare tisa na kupoteza mechi nane ikikusanya pointi 48.
Azam imekuwa na muendelezo wa kuuza wachezaji vijana kwenda nje kabla ya vijana hao watatu, hivi karibuni ilimuuza Arafat Ally kuitumikia ENNPI inayoshiriki Ligi Kuu Misri.
Chini ya kocha Mohamed Badru msimu uliopita timu hiyo ilimuuza Cyprian Kachwele kwenda Marekani ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Whitecaps FC 2 ya Canada.