KIUNGO mshambuliaji wa Kitanzania, James Damas anayekipiga MTV Wolfenbuttel U19 ya Ujerumani amesema huu ni msimu wake wa mwisho kuitumikia timu hiyo chini ya miaka 19.

James maarufu Rodrygo amekuwa kikosini hapo kwa takribani misimu mitatu akitokea Alliance ya Tanzania na alipata nafasi baada ya kufanyiwa majaribio.

Akizungumza na Mwanaspoti, James amesema huu ni msimu wake wa mwisho na mwakani atapandishwa timu ya wakubwa baada ya kufanya vizuri kwenye ligi ya vijana.

Ameongeza, benchi la ufundi la timu kubwa limevutiwa na kiwango chake baada ya kucheza mechi tisa akifunga mabao matano na asisti tatu.

“Bado nipo timu ya vijana U-19, lakini huu ndiyo msimu wangu wa mwisho na kuanzia mwakani nitapandishwa timu ya wakubwa kwa sababu ya umri umeshafikia sitaruhusiwa kucheza tena timu za vijana, pia kiwango kimewashawishi makocha,” amesema James na kuongeza;

“Timu iko nafasi ya pili na kwa kiasi kikubwa nimechangia mafanikio ya timu hadi sasa, nafikiri kwangu ni jambo zuri na litaenda kutimiza ndoto zangu za kucheza timu ya wakubwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *