BAADA ya Fountain Gate kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji, kocha wa kikosi hicho, Mohamed Laizer amesema haikuwa bahati yao huku akielekeza nguvu zake katika kuikabili Tanzania Prisons wikiendi ijayo.

Licha ya kupoteza mechi hiyo kwa bao 1-0, Laizer amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kiwango kizuri walichoonyesha hivyo anaamini mechi ijayo itakuwa fursa ya kuendeleza hilo na kufanya vizuri.

“Hatukupata tulichostahili. Tulicheza vizuri, tulipambana, lakini mpira una matokeo ya ajabu wakati mwingine,” amesema na kuongeza;

“Tunajua tulipo kimsimamo, lakini hatutaki kubaki hapo, mchezo (mechi) dhidi ya Prisons ni hatua nyingine ya kupanda. Tunakwenda kupigana.”

Rekodi zinaonyesha kuwa msimu uliopita timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, jambo linaloongeza msisimko wa mechi hiyo wikiendi ijayo.

“Sasa tuanaenda kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha makosa madogo tuliyoyaona Kirumba, tutapata matokeo mazuri mbele ya Prisons,” amesema.

Fountain Gate ilianza vibaya msimu huu wa ligi kwa kupoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya Mbeya City (1-0), Simba (3-0) na Mtibwa Sugar (2-0) kabla ya kujitutumua kwa kuichapa Dodoma Jiji na KMC kila mechi kwa bao 1-0 na kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Hivyo Laizer ana kibarua cha kuirejesha timu hiyo kwenye wimbi la ushindi wikiendi ijayo baada ya kutoka kuchapwa jijini Mwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Pamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *