LICHA ya kuwa na mabao matatu katika akaunti ya Ligi Kuu Bara, mshambuliaji wa Pamba Jiji, Peter Lwasa, amesema bado anaamini ana nafasi ya kuwa bora zaidi mbele ya lango kadri atakavyokuwa akipewa nafasi ya kucheza na kocha Francis Baraza.
Nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar na Gor Mahia ya Kenya aliyefunga mabao yote matatu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, anajiona ana nafasi ya kuboresha kiwango chake huku akishirikiana na wenzake ili kufunga mabao mengi zaidi.
“Nashukuru kwa hatua niliyoifikia, lakini najiona bado. Nafanya kazi kwa nguvu zaidi kila siku ili niwe bora na niwe hatari zaidi kwa mabeki,” amesema Lwasa.
Mabao hayo matatu yamemfanya Lwasa kulingana na Paul Peter na Salehe Karabaka wote wa JKT Tanzania na kuongoza orodha ya wafungaji wa Ligi kwa sasa.
Mabao yake ameyapachika kupitia mechi saba ilizocheza katika timu hiyo, ambapo mawili alitupia dhidi ya Mashujaa wakati Pamba ikishinda 2-1, kisha akafunga moja juzi dhidi ya Fountain Gate katika ushindi wa 1-0.
Kwa takwimu ya mabao manane ambayo Pamba Jiji imefunga hadi sasa katika Ligi Kuu kupitia mechi saba, Lwasa amechangia karibu nusu ikiwa ni sawa na asilimia 37.5.
Kwa mchango huo, mashabiki wa Pamba Jiji wameanza kumchukulia kama nguzo muhimu ya ushambuliaji, wakiamini bado kuna mambo makubwa yanakuja kutoka kwake.
Lwasa, hata hivyo, amesema hataki kubweteka na mafanikio ya mwanzo wa msimu, akieleza kuwa malengo yake ni makubwa kuliko idadi ya mabao aliyonayo sasa.
BARAZA ACHEKELEA
Katika hatua nyingine kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amechekelea kitendo cha timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya juzi kushinda dhidi ya Fountain Gate.
Baraza amewasifia wachezaji kwa kupambana na kuing’oa Mashujaa iliyokuwa inaongoza msimamo ikiwa na pointi 11 kabla ya Pamba kufikia 12 kupitia mechi saba.
“Ninachokiangalia zaidi kwa sasa si tu ushindi peke yake, bali mwendelezo wa kiwango cha timu, tukiweza hilo, tutakuwa bora zaidi kuliko sasa,” amesema kocha huyo na kuongeza;
“Pointi 12 hazimaanishi tumefika, ligi hii inabadilika kila wiki na kila mechi ni mtihani mpya, jambo muhimu ni kuendelea kupambana.”
“Nina imani na vijana wangu. Wakibaki na nidhamu hii na kuendelea kusikiliza na kufanyia kazi maelekezo, Pamba Jiji inaweza kumaliza ligi msimu huu ikiwa katika nafasi za juu.”
Hata hivyo, kocha huyo amesema bado wana kazi kubwa ya kufanya wikiendi ijayo ambapo watakuwa nyumbani tena kucheza dhidi ya KMC ambayo inapambana kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja.