NA leo tena! Ndivyo unavyoweza kusema wakati KMC iliyotoka kupasuka nyumbani katika mechi iliyopita mbele ya maafande wa JKT Tanzania, leo itashuka tena uwanjani kuvaana na Mtibwa Sugar iliyopoteza pia pambano lililopita la Ligi Kuu dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa KMC.
KMC inayonolewa na kocha Mbrazili, Marcio Maximo ikipoteza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu, itakuwa wenyeji wa Mtibwa iliyorejea katika ligi hiyo msimu huu, ambayo hata hivyo haijawahi kupata ushindi kwenye Uwanja wa KMC dhidi ya wenyeji wao hao.
Rekodi zinaonyesha katika mechi 12 ilizokutana tangu KMC ipande daraja mwaka 2018, Mtibwa imeshinda mara moja tu tena ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, lakini imepasuka mara saba na mechi nne zikiisha kwa sare tofauti na Wakata Miwa hao wakiwa hawana bahati ikiwa ugenini.
Hata hivyo, mechi ya leo ambayo ni ya pekee katika Ligi Kuu Bara inazikitanisha timu zenye hali tofauti, KMC ikionekana kuwa dhaifu zaidi kwani katika mechi saba ilizocheza imeshinda moja tu dhidi ya Dodoma Jiji, huku ikipoteza sita mfululizo.
Vijana wa Maximo pia wamefunga mabao mawili tu kupitia mechi hizo saba na wao kufungwa 11 wakiburuza mkia katika msimamo wakivuna pointi tatu tu, mbili pungufu na ilizonazo Mtibwa iliyopo katika nafasi ya 13 ikicheza mechi tano tu na kukusanya pointi tano.
Timu zote hazichekani katika udhaifu wa kufunga mabao, kwani hata Mtibwa imefunga mawili na kuruhusu matatu, ikishinda pia mechi moja kama KMC, isipokuwa yenyewe imetoka sare mbili na kupoteza mbili na zote ilipoteza kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Mtibwa ilianza kwa kufungwa mabao 2-0 na Yanga katika mechi yake ya mwisho wakati KMC ililala mwishoni mwa wiki mbele ya JKT kwa bao 1-0 na hivyo mechi ya leo kila timu itakuwa na kiu ya kutaka kujikomboa katika dakika 90 ili kuvuna pointi tatu muhimu.
Timu zote zitaendelea kutegemea wachezaji wengi chipukizi na wenye vipaji licha ya kuwepo na wazoefu watakaokuwa na kazi ya kusaka ushindi wa pili kwa kila timu na itakayozitumia vyema dakika 90 inaweza kutoka na furaha tofauti na ilivyokuwa katika mechi zao za mwisho.
Makocha wa timu hizo, Maximo kwa upande wa wenyeji na Mkenya Yusuf Chipo kwa Mtibwa, wana mtihani wa kuja na mbinu za kuwabeba kutatua tatizo la washambuliaji kushindwa kutumia nafasi zinazotengenezwa kuzalisha mabao.
Daruwesh Saliboko mwenye mabao mawili kwa upande wa KMC ataendelea kutegemewa kuibeba timu hiyo mbele ya mabeki wa Mtibwa, ambao nao watawategemea nyota kama Eric Kyaruzi, Nassor Kuziwa, Omari Marungu, Ibrahim Imoro na Onesmo Mayaya kulinda heshima ugenini.
Mtibwa iliyocheza mechi tano pia imeshinda moja, sare mbili na vipigo vipigo viwili.
Kwa namna timu hizo zinavyocheza na kasi ya wachezaji wanaotegemewa kuanzishwa katika mechi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa mashabiki watakaoenda uwanjani kushuhudia mechi hiyo wakapata utamu na burudani iwapo tu wachezaji wataamua kuliamsha kwa dakika zote 90 kuwania kurekebisha hali ya mambo.