BAADA ya Johannesburg Giants ya Afrika Kusini kuiondoa Dar City City katika nusu fainali ya mashindano ya kikapu Road to BAL Elite 16, kocha wa timu hiyo, Florsheim Ngwenya amesema walicheza na timu nzuri iliyokuwa na wachezaji wenye viwango bora Afrika.
Pamoja na ushindi wao huo, amesema watu wengi hawakuipa nafasi timu yake kushinda akisema wapinzani wao walikuwa bora na kila shabiki aliamini kwamba walikuwa wameukamata mchezo na hivyo lolote zuri lingekuwa upande wao.
Katika mchezo huo Johannesburg Giants iliishinda Dar City kwa pointi 71-69 katika nusu fainali iliyofanyika kwenye uwanja wa ndani wa Karasani mjini Nairobi, Kenya. Hata hivyo ushindi wa timu hiyo ulipatikana baada ya pointi 20 kufungwa katika robo ya tatu na kabla ya hapo Dar City ilikuwa inaongoza kwa 39-34.
“Tulifanikiwa kupata nafasi kadhaa baada ya kubadili safu ya ulinzi ya namba 2 (shooting guard) na 3 (small forward). Tulifanikiwa kuwatuliza wafungaji wao wa pembeni mpaka tukapata ushindi,” amesema Ngwenya.
Sababu nyingine iliyofanya Dar City ipoteze mchezo huo ni kutokana na madhambi iliyofanya mara tano ndani ya dakika ya 3 ya robo ya nne jambo lililoifanya Johannesburg Giant itumie nafasi hiyo kufunga pointi.
Iko hivi, timu inapapata nafasi ya kufunga mipira adhabu endapo iliyofanya madhambi mara tano ikifanya eneo lolote la uwanja, kwani mpira unachukuliwa na timu inapewa irushe mitupo miwili katika goli la mpinzani.
Dar City ingeshinda endapo ingetumia nafasi vizuri ilizopata za kufunga katika robo ya nne ya dakika ya 4, 6, 8.
Katika mchezo huo Dar City ilianza kuongoza robo ya kwanza kwa pointi 21-13, 18-24, 14-20, 16-17.
Katika mashindano hayo Dar City ilishika nafasi ya tatu baada ya kuifumua Ferroviario da Beira ya Msumbiji kwa pointi 92-77. Nayo Nairobi City Thunder iliishinda Johannesburg Giants katika fainali ya mashindano kwa pointi 92-82 na kufanya timu hizo mbili zitinge robo fainali ya BAL Elite 16. Timu hizo zitaungana na zingine sita zilizofanya vizuri katika maeneo mengine.
NISRE, SIBANYONI WALIVUTIA
Katika mashindano hayo nyota Nisre Zouzoua wa Dar City na Nkosinathi Sibanyoni wa Johannesburg Giants walikuwa kivutio.
Zouzoua anayecheza kama ‘shooting guard’ ubora wake ulionekana alipokuwa akicheza nafasi zote uwanjani na kuwafanya wapinzani wao wapambane kumdhibiti.
Nyota huyo aliyecheza dakika 40 bila kupumzika, ubora wake aliuonyesha pia katika ufungaji kwenye eneo la mtupo mmoja wa ‘three points’ pamoja na eneo la pointi mbili.
Mchezaji huyo alishirikiana vizuri na wachezaji wenzake Hasheem Thabeet, Amin Mkosa, Solo Diabate na Deng Angok kuhakikisha wanashinda mchezo, lakini bahati haikuwa upande wao.
Katika mchezo huo Zouzoua aliongoza kwa kufunga pointi 25, akidaka mipira ya rebaundi 13, asisti nane, kuzuia mara nne na kupokonya mipira mara tatu. Kwa upande wa Sibanyoni aliyeonekana kuwa mwiba kwa Dar City alicheza akili ya ajabu wakati amebanwa akionekana akitoka nje ya eneo la ufungaji la pointi mbili na kufunga.
Katika mchezo huo alifunga pointi 21 akidaka ribaundi mara 14, asisti nne, kuzuia mara moja na kupokonya mipira mara mbili. Wachezaji wengine walioonyesha viwango bora ni Solo Diabate, Raphiael Putney, Deng Angok (Dar City), Chase Adams (Nairobi City Thunder), Omar Thielemans (Matero Magic), Jovan James na Tony Dribela (Namuwongo Blazers) pamoja na Joshua Thomas wa Ferroviario da Beira.