
MSHAMBULIAJI wa Simba anayecheza JKT Tanzania kwa mkopo, Valentino Mashaka amesema kwa sasa anachotaka ni nafasi tu ndani ya kikosi hicho ili kuonyesha ubora wake.
Valentino ambaye alisajiliwa Simba msimu uliopita akitokea Geita Gold, huku akimwaga wino wa miaka mitatu kuwatumikia mabosi hao wa Msimbazi, anaitumikia JKT Tanzania kwa mkopo wa msimu mmoja.
Wakati msimu huu akiwa bado hajafunga, msimu uliopita akiwa Simba alifunga mabao mawili Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mashaka alisema hajaonekana uwanjani kwa muda hata alipofika JKT kwa sababu kuna mambo alikuwa akiyaweka sawa.
Alisema kuwa kwa sasa mchawi ni nafasi tu kikosni kwani tayari eneo analochezea kuna mastaa aliowakuta na wanafanya vizuri.
“Nafasi yangu ni nzuri kwa hiyo kila timu ninayokwenda lazima iwe na ushindani wa namba, ila mimi kama mchezaji natakiwa kupambana ili niweze kucheza. “Sijaanza bado kucheza kwa sababu kuna mambo yangu hayakukaa sawa, ila naona waliopo walivyo wa moto kwa hiyo ni ngumu kuanza kucheza kwa sababu tayari walishaonyesha kitu.”
JKT Tanzania inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi saba, ikishinda mbili, sare nne na kupoteza mmoja, huku leo saa 12:15 jioni ikiikaribisha TRA United kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo, Dar es Salaam.