PAMBA Jiji imevunja rekodi ya msimu uliopita ndani ya raundi saba za kwanza Ligi Kuu Bara kiasi cha kuwaibua wakongwe wa timu hiyo akiwemo Khalfan Ngassa.

Pamba ambayo kwa sasa ni kinara Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 12, msimu uliopita ndani ya mizunguko saba ya kwanza ilikuwa haijaonja ushindi wa kwanza katika ligi.

Msimu uliopita ilianza kwa sare na Tanzania Prisons (1-1), Dodoma Jiji (0-0), Azam (0-0), Mashujaa (2-2), ikafungwa na Singida Black Stars bao 1-0, Coastal Union mabao 2-0 na Yanga 4-0.

Hivyo ndani ya raundi saba za mwanzo ilivuna pointi nne tofauti na sasa ambapo imejikusanyia 12.

Ngassa aliyeutamba na Pamba miaka ya 80, alisema: “Inapendeza kuona timu yetu ya Mwanza ikianza vizuri msimu, inatukumbusha miaka yetu ya zamani tulimudu kushindana na klabu yoyote ile, hatukuwa na hofu.”

Aliongeza kuwa wachezaji wanatakiwa kujitoa zaidi ili kuendelea kufanya vizuri na ikiwezekana wamalize ligi wakiwa nafasi ya juu tofauti na msimu uliopita waliposhika ya 11 wakiwa na pointi 34.

Kwa upande wake, Seleman Kigi, alisema: “Kuna mechi nane mbele kama unaweza kukusanya angalau pointi 12 nyingine, jumla ni 24, tutakuwa salama zaidi huku tukisubiri duru ya pili.”

Ndani ya mechi 15 msimu uliopita Pamba ilikusanya pointi 12 ambazo msimu huu imezipata ikicheza mechi saba. Katika historia msimu ambao Pamba Jiji ilifanya vizuri zaidi Ligi Kuu ilikuwa 1990 ilipotwaa ubingwa huku mafanikio mengine makubwa ni 1989 na 1992 ilipotwaa Kombe la Nyerere.

Pamba Jiji ilianzishwa 1968 iki ni miaka 57 sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *