BAADA ya Simba kupoteza mechi ya kwanza hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, unaambiwa ndani ya klabu hiyo moto umewaka, huku mabosi wa wekundu hao wakimpa sharti gumu kocha Dimitar Pantev wakitaka ashinde mechi ijayo, la sivyo kibarua kinaota nyasi.

Simba ambayo inatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo jijini Dar kwa mechi za nyumbani michuano ya kimataifa msimu huu, Jumapili ya Novemba 23, 2025 ikiwa hapo ilichezea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico kutoka Angola.

Mechi hiyo iliwafanya mabosi na mashabiki wa Simba kunyong’onyea, huku wengi wakidai kwamba, shida ilianza kwenye upangaji wa kikosi.

Malalamiko mengi yalikwenda kwa Pantev ambaye anaonekana kuwa ndiye mwenye kauli kubwa kwenye benchi la ufundi la Simba kuliko Seleman Matoka ingawa kwenye makabrasha anatambulika kama kocha msaidizi na Matola ndiye mkuu.

Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa, baada ya kupata matokeo mabaya viongozi walitaka kumfukuza kocha huyo ila wakaamua kuzungumza naye kwanza.

Chanzo cha taarifa kilisema wengi walihuzunishwa na namna alivyokipanga kikosi kama kinakwenda kucheza mechi ndogo wakati ni michuano ya kimataifa, hivyo ili kusahihisha makosa hayo, hana budi kuiandaa timu ishinde dhidi ya Stade Malien.

“Ilikuwa lazima tukutane naye, hali si mmeiona sio nzuri, hakuna anayeweza kuyapokea matokeo yale kirahisi, lazima tuchukue hatua.

“Kuna mambo mengi kwa sasa dhidi ya kocha, tulianza sisi kama viongozi kuyaona, lakini sasa yamewafikia hata mashabiki wakipiga sana kelele.

“Tumekutana naye tumemwambia salama yake ni kufanya mambo yabadilike kwa haraka tunapokwenda kucheza na Stade Malien,”  kilisema chanzo cha taarifa kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa bodi ya Simba.

Kiliongeza kuwa. “tunataka kuona mambo yanabadilika haraka tena kuanzia mchezo unaofuata dhidi ya Stade Mallien, kinyume na hapo itakuwa ngumu kuvumilika, ili tusifike kwenye maamuzi ambayo hayatamfurahisha ni bora asikilize na kubadilisha mambo.

“Kocha ana timu yenye wachezaji ambao wanaweza kumtengenezea matokeo, sasa kazi ni kwake, imefikia hatua hata wachezaji wanalalamika kwamba wanajiona kama hawana thamani, hawapewi muda stahiki wa kuitumikia Simba.”

Simba itakuwa nchini Mali Jumapili ijayo Novemba 30, 2025, ikiwa ni mechi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien, ambayo ilitoka suluhu na Esperance.

Wakati Simba inapoteza mechi hiyo ya kwanza Kundi D ikiwa nyumbani, kikosi hicho kilianza bila ya mshambuliaji halisi namba tisa, badala yake ikawatumia viungo washambuliaji wanne, Joshua Mutale, Morice Abraham, Neo Maema na Elie Mpanzu. Steven Mukwala, Jonathan Sowah na Seleman Mwalimu ambao ni washambuliaji, walikuwa benchi.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya nne mfululizo kwa Simba kushindwa kupata ushindi nyumbani katika michuano ya CAF kwani awali ililazimishwa sare tatu kuanzia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita dhidi ya RS Berkane (1-1) na mechi mbili za raundi ya awali kwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana (1-1) na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini (0-0). Kesho Alhamisi, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri kuifuata Stade Malien nchini Mali kwa ajili ya mechi ya pili ya kundi hilo itakayopigwa Jumapili mjini Bamako ikihitaji kupata ushindi ili kujiweka pazuri katika Kundi D lenye mabingwa wa zamani wa Afrika, Esperance ya Tunisia waliolazimishwa suluhu nyumbani na Stade Malien.

Endapo Simba itashindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Stade Malien, kuna uwezekano Pantev asiwepo na kikosi hicho wakati timu hiyo ikikabiliana na TRA United, Desemba 3, 2025 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabiora na kufunga hesabu za mwaka 2025 dhidi ya Azam Desemba 6, 2025. Mechi zote zikiwa ni za Ligi Kuu Bara. Pantev raia wa Bulgaria, alitambulishwa Simba Oktoba 3, 2025, ikiwa ni siku chache baada ya kuachana na Fadlu Davids, aliyeiongoza timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *