Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC imeahirisha kikao cha marais kilichopangwa kufanyika mwezi huu hadi Januari mwakani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Vyanzo kutoka Arusha vimethibitisha mabadiliko hayo ingawaje hakuna maelezo yaliyotolewa ya kusogeshwa mbele kikao hicho.
Kongamano hilo lilitarajiwa kufanyika Nairobi ambayo inashikilia uenyekiti , Rais William Ruto ambaye amekuwa mwenyekiti wa EAC akitarajiwa kukabidhi uongozi kwa nchi ya Somalia iliyojiunga na Jumuiya hiyo hivi majuzi.

Kuahirishwa kwa kikao hicho kunajiri wakati huu,Jumuiya hiyo ikikabiliwa na mivutano ya kisiasa ,usalama mdogo na ugumu wa kutekeleza swala la utangamano.
Nchi ya Sudan Kusini ,imekuwa kwenye hali tete baada ya kukamatwa kwa makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimekuwa kwenye mvutano mkubwa kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 wameendelea kuchukua maeneo mapya na kuendeleza mapigano na vikosi vya serikali na washirika wake ,licha ya makubaliano ya amani ya Doha.
Tanzania pia imetoka kwenye machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 29 ,huku kukiwa na shinikizo kutoka jamii ya kitaifa kwa mamlaka nchini humo kuwajibika kufuatia mauaji ya raia wakati wa vurugu hizo.
Aidha ukanda huu umekuwa kwenye mizozo ya kibiashara kati ya nchi wanachama.