DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya GSM Group imeingia hatua mpya ya kihistoria baada ya kupokea magari 100 ya kusafirishia mafuta kutoka kampuni ya malori Sino truck Tanzania hatua inayotajwa kuongeza ufanisi katika mnyororo wa usafirishaji nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya mapokezi Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni za GSM, Benson Mahenya, alisema ujio wa magari hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni hiyo kupanua usafiri wa mafuta nchini na nje ya mipaka.

“Leo ni siku ya kihistoria kwetu. Tumepokea magari 100 ya mafuta ikiwa ni awamu ya kwanza, na ndani ya siku 20 zijazo tutapokea mengine 100 kukamilisha mpango wetu wa kuwa na magari 200 kabla ya mwaka huu kuisha,” alisema Mahenya.

Mahenya alifichua kuwa ushirikiano kati ya GSM na kampuni ya malori na ya mafuta Sinotruk, umekuwa wa muda mrefu na wenye mafanikio makubwa.

“Tangu tulete magari yetu ya kwanza tumeshanunua jumla ya magari 1,630 ya ujazo tofauti—tani 3, 5, 7 na 30. Kadiri siku zinavyokwenda tunaendelea kufanya biashara nao kwa sababu magari haya ni uti wa mgongo wa uchumi,” alisema.

Alibainisha kuwa magari hayo yanachochea ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha mafuta, bidhaa ghafi na bidhaa zilizokamilika ndani ya Tanzania, kwenda nchi jirani na kurudi, hivyo kuchangia katika muingiliano wa biashara kikanda.

Mahenya alisema hapo nyuma GSM haikuwa kwenye biashara ya kubeba mafuta, lakini kupitia mpango wa muda mrefu, wameweza kuingia rasmi kwenye sekta hiyo na kuleta chapa mpya ya HOWO, na GSM ndiyo ya kwanza kuileta nchini.

Kwa upande wake, Sun Yang Yang, Meneja Mkuu wa Sino Truck Tanzania, alisema uhusiano kati ya kampuni hiyo na GSM umejengwa juu ya uaminifu na matarajio ya muda mrefu.

“Tangu 2021, GSM imenunua zaidi ya magari 1,000 kutoka kwetu. Huu ni ushahidi wa imani kubwa waliyo nayo kwa bidhaa zetu,” alisema.

Aliongeza kuwa Sino Truck inatarajia kufungua kiwanda cha pili nchini ifikapo 2026, hatua inayotarajiwa kuleta ajira zaidi ya 200 na kuchochea ukuaji wa sekta ya magari na vipuri nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *