MWANZA: WAHITIMU wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Mwanza wametakiwa kuchangamkia na kutumia fursa zilizopo katika Mkoa wa Mwanza ili kujiletea maendeleo na kuchangia katika ustawi wa Taifa.
Rai hiyo imetolewa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya, wakati akihutubia mahafali ya 23 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Mwanza.
Balandya alisema wahitimu wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, hususan katika maeneo yenye fursa kubwa za kiuchumi ndani ya mkoa huo.
“Wahitimu mkitumia vyema ubunifu na elimu mliyoipata mtapiga hatua kubwa sana. Mkoa wa Mwanza una fursa nyingi ikiwemo ufugaji wa samaki kwa vizimba, uvuvi pamoja na kilimo,” alisema Balandya.

Jumla ya wahitimu 1,035 wametunukiwa vyeti katika ngazi ya cheti cha awali, astashada na shahada katika mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Mwanza.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mtendaji Mkuu wa TIA nchini, Prof William Pallangyo, alisema idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hatua inayoonesha kuimarika kwa chuo hicho katika utoaji wa elimu bora.

Alisema mwaka 2012 TIA Kampasi ya Mwanza ilianza na wanafunzi 381, na kufikia mwaka 2024 idadi hiyo imeongezeka hadi wanafunzi 1,328, jambo linalodhihirisha ongezeko la uhitaji wa elimu ya uhasibu na usimamizi wa biashara.
Profesa Pallangyo alisema chuo kitaendelea kuwekeza katika elimu ya vitendo na kuongeza ufanisi kwa wanafunzi, ambapo kwa sasa ujenzi wa miundombinu mbalimbali unaendelea ikiwemo hosteli za wanafunzi na canteen ya chuo.
“Kwa sasa hosteli zimefika asilimia 70 na zinatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 7.2 hadi kukamilika. Canteen imefikia asilimia 4 na itagharimu shilingi milioni 351, na inatarajiwa kukamilika mwaka 2026,” alisema.

Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu, hatua iliyowezesha ongezeko la wanufaika kutoka 741 mwaka 2024 hadi 1,299 mwaka 2025 katika kampasi hiyo.
Profesa Pallangyo alibainisha kuwa Kampasi ya Mwanza imeanzisha kozi mpya ya Usimamizi wa Biashara kuanzia ngazi ya cheti hadi astashada, ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa taaluma zinazotolewa na TIA.
Pia alisema kuwa kampasi hiyo imefanikiwa kufanya na kuchapisha utafiti 21 katika masuala ya uchumi, fedha na uongozi, hatua inayolenga kuongeza mchango wa TIA katika kuleta maendeleo nchini.