DAR ES SALAAM: WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji imeiagiza Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) kuhakikisha inavutia uwekezaji wenye thamani ya Dola bilioni 15 na kusajili miradi angalau 1,500 katika skimu zote za uwekezaji nchini ili kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Agizo hilo limetolewa leo Novemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TISEZA na Bodi ya Mwongozo wa Watoa Huduma kwa Wawekezaji (ISPs) ambapo amesema Dira ya 2050 inatambua kuwa uchumi imara na endelevu unategemea na kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kuwekeza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo amesema serikali inakamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (MKUMBI II), ambao utatumika kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kwamba mkakati huo unalenga kuongeza ushindani wa nchi katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
SOMA ZAIDI: Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji- Tiseza
Ameeleza kuwa vigezo muhimu vinavyotumika kuvutia uwekezaji ni pamoja na uimara wa taasisi, utawala wa sheria, utulivu wa kisiasa, uwepo wa soko, upatikanaji wa mitaji na fursa mbalimbali kama kilimo, viwanda, madini na nishati. Pia amesema Dira ya Taifa ya 2050 imeweka msukumo katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kutumia fursa za kijiografia kukuza uchumi.
Aidha, katika kueleza mikakati ya serikali ya kuongeza uwekezaji, Profesa Mkumbo amesema kutaanzishwa kituo maalumu cha kuhudumia wawekezaji vijana, kuanzishwa kwa programu ya kuwawezesha vijana kuanzisha viwanda, kusogeza huduma za TISEZA katika kila mkoa ifikapo mwaka 2028 na kuanzishwa kwa vivutio vipya vya uwekezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amesema mamlaka hiyo itahakikisha ubunifu katika utoaji wa huduma na kutoa kipaumbele kwa wawekezaji vijana, ikiwemo kutenga maeneo maalumu na kuwasaidia kuanzisha miradi inayoweza kuzalisha ajira.

Wawekezaji waliohudhuria hafla hiyo wameipongeza serikali kwa kuzindua Bodi ya Mwongozo wa Watoa Huduma kwa Wawekezaji, huku wakisema kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini,endapo Dira ya 2025 ikitekelezwa itawapa ujasiri wa kuongeza mitaji yao nchini.