Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hali hasasi na nyeti iliyopo hivi sasa katika Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza kwamba: “wakati maadui wa pamoja wa mataifa ya Kiislamu wanatafuta njia za kuzidisha mashinikizo, ingetarajiwa nchi za Kiislamu zirahisishiane hali na mazingira na kujiepusha na utatizaji wa mambo”.

Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan yaliyofanyika jana usiku hapa mjini Tehran, ambapo sambamba na kuashiria masuala ya pamoja ya historia, utamaduni, na uhusiano wa kiudugu wa muda mrefu uliopo kati ya Iran na Uturuki ameeleza kwamba, uhusiano huo umekita mizizi, ni wa dhati, na wenye fursa nyingi za kustawishwa; na akaongezea kwa kusema: “ikiwa nchi za Kiislamu zitachukua hatua kwa irada na utashi wa pamoja uliofungamana na umoja, muelekeo mmoja, na kubadilishana uzoefu na tajiriba, hakuna dola lolote litakaloweza kuyakwamisha mataifa ya Kiislamu”.

Akizungumzia tajiriba na uzoefu wa Ulaya, Rais wa Iran amekumbusha kuwa, licha ya kuwa na historia ndefu ya vita na migogoro, nchi za Ulaya leo zimeweza kuhafifisha mipaka yao, kuunda miundo ya pamoja ya kifedha na kisiasa, na kuunganisha mitandao yao ya biashara na usafirishaji; na akabainisha kuwa: kutokana na Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na mambo mengi zaidi ya pamoja ya kiutamaduni na kiustaarabu yanayofanana, ikiwa yataweka kando tofauti na kufuata mkondo wa ushirikiano thabiti na maendeleo ya pamoja, utaweza bila shaka yoyote kusonga mbele kupitia uunganishaji wa mitandao ya biashara, utaalamu, na utamaduni.

Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian ameashiria pia hali nyeti na hasasi iliyopo hivi sasa katika Ulimwengu wa Kiislamu, na akasema: “wakati maadui wa pamoja wa mataifa ya Kiislamu wanatafuta njia za kuzidisha mashinikizo, ingetarajiwa nchi za Kiislamu zirahisishiane hali na mazingira na kujiepusha na utatizaji wa mambo. Sisi ni ndugu na kuna ulazima wa kustawisha uhusiano wetu, na tunaamini kwamba ugaidi na silaha havitaweza katu kuvuka mipaka inayopita ndani yake biashara, sayansi, na utamaduni”.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amewasilisha salamu maalumu za Rais wa nchi yake kwa Dakta Pezeshkian na ujumbe wake maalum kuhusu umuhimu wa kupanua ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi, na kikanda kati ya nchi mbili…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *