Wahamiaji wa Kiafrika wakila kiapo cha uraia wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi,

Takriban nchi kumi za Afrika zimejikuta katika hali ya sintofahamu baada ya Rais Donald Trump kuagiza kufanyike mapitio ya haraka na ya kina kuhusu taratibu za uchunguzi kwa waombaji wa Kadi ya Kijani (Green Card), kufuatia shambulio lililowahusisha wanachama wa Jeshi la Akiba la Taifa la Washington D.C.

Rais wa Marekani Donald Trump alitoa tamko hilo kufuatia tukio lililotokea karibu na Ikulu ya White House jijini Washington mnamo Jumatano (Novemba 26).

Katika hotuba yake, alitangaza azma ya kuweka marufuku ya kudumu kwa raia wa “nchi za ulimwengu wa tatu” kuingia nchini Marekani.

Marekani, ikiwa miongoni mwa mataifa tajiri zaidi duniani, iliweka na kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) halisi la Marekani kwa mwaka 2025 ikikadiriwa kuwa kati ya asilimia 1.9% na 2.5%.

Hali inayofanya iwe kivutio kikubwa kwa wahamiaji wanaotafuta fursa za kiuchumi na maisha bora.

Raia wengi kutoka mataifa mbalimbali huwasili Marekani kama wakimbizi, wanafunzi, watalii au wafanyabiashara.

Hata hivyo, mara wanapoingia nchini humo, wengi hutafuta hadhi ya kufanya kazi na kuishi kama raia wa kawaida.

Kadi ya Kijani, inayotoa hadhi ya ukaazi wa kudumu, imekuwa mojawapo ya njia maarufu zaidi kwa waafrika wengi wanaotaka kuboresha maisha yao nchini Marekani.

Baada ya tangazo la Trump, maswali yanaulizwa, Ulimwengu wa Tatu ni nini haswa? Nchi zipi ziko ndani yake? Je, Tanzania ni miongoni mwao?

Soma pia:

Kwa mujibu wa mwongozo mpya, USCIS sasa inaweza kuzingatia “hoja hasi zinazohusiana na nchi husika” katika kuchakata maombi ya ‘Green Card’ kutoka kwa raia wa nchi 19 ikiwemo 10 za Afrika.

Zuio hilo limegawanywa kwa sehemu mbili, zuio kamili na zuio sio kamili.

Zuio kamili ina maana kwamba raia wa nchi hizo hawaruhusiwi kuingia Marekani hata kama wana visa au wanapanga kuomba visa au Green Card; visa za aina zote zimezimwa.

Zuio kiasi (partial restrictions) ina maana kwamba baadhi ya visa, hasa za kawaida (watalii, wanafunzi, wageni), na visa ya wahamiaji mpya, vimezimwa au vimewekwa masharti magumu.

Hata hivyo, baadhi ya visa maalumu, au visa zilizotolewa kabla ya tarehe ya 9 Juni 2025, inaweza kutambuliwa.

Nchi za Afrika zenye marufuku kamili ya kuingia Marekani

Hafla ya kuwaapisha wahamiaji

Chanzo cha picha, Getty Images

Chini ya tamko jipya la Rais wa Marekani, raia wa nchi zifuatazo za Afrika wamewekewa marufuku kamili ya kuingia Marekani:

  • Chad
  • Jamhuri ya Kongo (Republic of the Congo)
  • Guinea ya Ikweta (Equatorial Guinea)
  • Eritrea
  • Libya
  • Somalia
  • Sudan

Marufuku haya yanawahusu watu walio nje ya Marekani kuanzia tarehe 9 Juni 2025, na wasio na visa halali ya Marekani iliyotolewa kabla ya tarehe hiyo.

Nchi za Afrika zenye marufuku kiasi

Nchi zifuatazo zimewekewa vikwazo vya kiasi wakitaka kuingia Marekani:

  • Burundi
  • Sierra Leone
  • Togo

Raia wa mataifa haya wanakabiliwa na masharti na vizuizi vinavyoathiri aina fulani za visa, ikiwemo:

  • Visa za wahamiaji

Baadhi ya visa zisizo za wahamiaji, kama vile:

  • B-1/B-2 (ziara na shughuli za muda mfupi)
  • F (wanafunzi)
  • M (mafunzo ya ufundi)
  • J (programu za kubadilishana wanafunzi au wataalamu)

Marufuku haya ya sehemu hayamaanishi kuwa safari zote zimezuiwa, lakini yanaweka ukomo mkubwa katika visa zinazotumika mara kwa mara, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kusafiri au kuingia Marekani kwa waombaji wengi.

Nchi nyingine zilizo kwenye orodha

Kadi ama kibali hiki cha kisasa kabisa kinachotolewa na Marekani kinakuwa na vitu muhimu kama Majina, aina ya kibali hivyo, tarehe ya kuzaliwa, nchi uliozaliwa, jinsia yako, picha na alama za vidole. Inafanana tu kimuundo kama kitambulisho cha taifa, ama kadi za benki zenye taarifa muhimu za mtumiaji.

Chanzo cha picha, Getty Images

Afghanistan, Myanmar, Cuba, Haiti, Iran, Laos, Turkmenistan, Venezuela na Yemen.

Kupitia mtandao wa X, Mkurugenzi wa USCIS, Joseph Edlow, alisema Trump ameagiza:

“Uchunguzi mkali wa kila Kadi ya Kijani ya raia yeyote kutoka nchi yoyote yenye wasiwasi.”

Alisisitiza kuwa kulinda wananchi wa Marekani ni suala la kipaumbele, na akadai kuwa Wamarekani hawapaswi “kubeba gharama za sera zisizo makini za utawala uliotangulia.”

Je, Tanzania imeorodheshwa?

Ingawa Tanzania haijatajwa kuwa nchi zinazotathminiwa upya kado ya kijani, raia wanaoomba visa watagharamika zaidi.

Awali, iliripotiwa kuwa serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump, imeiondoa Mali katika orodha ya nchi zinazowekewa dhamana ya visa.

Hata hivyo, imeendelea kuziorodhesha Tanzania, Malawi, Gambia, Mauritania, pamoja na São Tomé and Príncipe.

Raia wa mataifa haya wanalazimika kulipa dhamana ya hadi dola 15,000 sawa na takribani TSh milioni 38.95 wanapoomba visa ya Marekani.

Ofisi ya Upelelezi wa Jinai katika jijini Nairobi inachunguza mamia ya malalamiko kuhusu mashirika yanayodai kuwatafutia watu ajira

Chanzo cha picha, Getty Images

Athari kwa bara la Afrika

Athari kwa bara la Afrika zinatarajiwa kuwa kubwa.Marekani ni miongoni mwa maeneo makuu yanayowavutia wahamiaji wenye ujuzi, wanafunzi, na wakimbizi kutoka Afrika.

Masharti mapya yanaweza kuongeza ucheleweshaji wa vibali, kufunga milango ya uhamiaji, na kuongeza wasiwasi miongoni mwa familia zilizo katika hatua mbalimbali za maombi ya kadi kijani ‘Green Card’.

Hatua hii inaashiria kurejea kwa sera zinazotumia visingizio vya usalama wa taifa ambavyo mara nyingi huathiri zaidi mataifa ya Afrika kuliko maeneo mengine.

Mataifa kama Somalia, Eritrea na Sudan tayari yanakabiliwa na masharti makali ya uhamiaji, na agizo hili linaweza kuzidisha ugumu huo kwa muda mrefu.

Kwa serikali za Afrika, hili linazua changamoto mpya katika diplomasia na majadiliano na Marekani.

Kwa wahamiaji wa Kiafrika, linaongeza hali ya sintofahamu katika kipindi ambacho uhamaji, ajira za kimataifa na uhamishaji fedha kutoka waafrika walioko Marekani ni nguzo muhimu za uchumi barani Afrika.

Utekelezaji wa agizo hili unaanza lini?

Sera hii inahusu maombi yote yanayoendelea na yale yatakayowasilishwa kuanzia Novemba 27, 2025.

USCIS itakuwa na uwezo mpana wa kuchelewesha maamuzi, kukataa maombi, au kuhitaji uthibitisho wa ziada kutoka kwa waombaji wa kadi ya kijani.

Trump alitangaza kuwa Sarah Beckstrom mwenye umri wa miaka 20 amefariki kutokana na majeraha yake, huku Sajenti Andrew Wolfe akiwa bado katika hali mahututi.

Akiita tukio hilo “shambulio la kigaidi,” Trump alikanusha taarifa kwamba mshukiwa alikuwa na uhusiano wowote na mashirika ya ujasusi ya Marekani.

Inapatikanaje kadi hii na je ni rahisi kuipata?

Kibali hiki kinatolewa kwa watu wasio raia wa Marekani baada ya kutimiza taratibu na kupata sifa zinazopaswa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Neno Green Card’ linatumika zaidi Marekani labda kwa kuwa kadi hiyo ina rangi ya kijani, kwa nchi nyingine kibali hicho wanaita kitambulisho cha mkazi. Kwa mfano Ujerumani wanaita Aufenthaltgenehmigung’.

Kwa mujibu wa baadhi ya raia wa kigeni waliopata kadi hiyo wanasema unaweza kuipata kwa jasho kiasi, sio rahisi kama ambavyo wengi wanadhania.

“Imenichukua miaka 15 kujaribu kuwa raia wa Marekani, kupitia Kadi hii. Lakini nimeshindwa’, anasema Yarzidu, sio jina lake halisi raia wa Palestina.

Zipo njia saba maarufu zinazoweza kukuwezesha kupata Kadi hii.

Ya kwanza kubwa na inayotumika sana hutolewa kwa familia, kwa maana ya kwamba ukioa ama kuolewa na raia wa Marekani unapewa kibali hiki, na inaweza kukuchukua mpaka mwaka kukipata.

‘Nililazimika kutafuta mwanamke na kuoa, nikiacha mwanamke wangu nyumbani (Tanzania), nikajifanya sijaoa, nikafanikiwa kupata, yote ni kutafuta maisha, anasema Omary (sio jina lake halisi), aliyepata kadi hiyo mwaka 2020.

Njia ya pili ni kwa kuwekeza kibiashara nchini humo kupitia mtaji wa angalau dola nusu milioni mtaji ambao baada ya mwaka mmoja unaweza kufikia dola 900,000.

Pia unaweza kupata kibali hiki kama umeenda kufanya kazi nchini humo. Mwajiri wako anapaswa kuwa raia wa Marekani na kampuni yake imefanya kazi kwa angalau mwaka mmoja. Njia hii inaonekana rahisi zaidi na inakimbiliwa zaidi kwa watu wenye fursa ya ajira kwa makampuni ya huko.

Unaweza pia kupata kibali kwa njia ya kusoma au kwa wale ambao ni raia wa kigeni waliopata mafanikio ya kutukuka mfano Drake au Ryan Renolds ambao mafanikio yao yanawapa fursa ya kupata kadi hii kirahisi.

Ukishinda tuzo kubwa kama za Oscar, Grammy, ama Pulitzer kupata kibali hiki ni rahisi zaidi na njia nyingine inayotumika sana ni kupata kupitia bahati nasibu inayoweza kumdondokea mtu yeyote aliyejaza fomu kupitia njia mbalimbali za mitandao na kujaribu bahati yake.

Kwa mwaka, kuna watu zaidi ya 55,000 huomba kadi hii kwa njia ya bahati nasibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *