
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi yetu amesema kuhusu vitendo vya Marekani dhidi ya amani ya dunia kuwa, ukweli ni kwamba Marekani ni tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa, na hivi sasa tunashuhudia matumizi maovu ya nguvu za Marekani katika nchi kama Venezuela na Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Ismail Baghaei, amesema hayo wakati akijibu maswali katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari. Baghaei amesema: Suala muhimu zaidi katika eneo la Asia Magharibi linaendelea kuwa ni vitisho vya kiusalama vinavyosababishwa na jinai za utawala wa Kizayuni na ukiukaji wake mkubwa wa sheria za kimataifa dhidi ya Palestina, Lebanon na Syria. Licha ya kusitisha mapigano nchini Lebanon na Ghaza, lakini Israel inaendelea kukiuka makubaliano hayo kwa uwazi kabisa. Huko Ghaza, idadi ya vitendo vya utawala wa Kizayuni vya kutoheshimu makubaliano ya kusisitisha vita imefikia karibu matukio 600 na kila ukiukaji wa makubaliano hao unakwenda sambamba na mauaji ya watu wasio na hatia. Kwa bahati mbaya, mashirika ya kimataifa yameshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuitia adabu Israel.
Amma kuhusu kitendo cha Marekani cha kuzitishia nchi za dunia zisishiriki katika mkutano wa G20 wa Afrika Kusini, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Ukweli ni kwamba Marekani ndilo tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa. Tunashuhudia matumizi ya nguvu za wazi za Marekani huko Venezuela na pia kutoa vitisho dhidi ya Afrika Kusini na dhidi ya nchi zote zilizoshiriki kwenye mkutano wa kilele wa G20. Amma kuhusu ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia hapa Tehran, Baghaei amesema: Ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia ni mwendelezo wa mchakato ulioanza miaka miwili iliyopita wa kustawisha uhusiano wa Iran na Saudia na kuongeza ushirikiano wa kutatua masuala mbalimbali kama ya Palestina, Lebanon na Syria.