ZANZIBAR : RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa kimataifa kutokana na uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji zinazohitaji nguvu ya wadau na taasisi za nje.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipokutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Commonwealth Enterprise and Investment Council (CWEIC), Lord Swire, na ujumbe wake waliofika kwa ajili ya mazungumzo ya ushirikiano.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya mageuzi makubwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kwa lengo la kuvutia wawekezaji hususan katika sekta mbili kuu za Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo zinazochangia takribani asilimia 30 ya pato la taifa.

Rais Mwinyi amesema ujio wa ujumbe huo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Zanzibar na taasisi za kimataifa, na kwamba fursa zilizopo zinahitaji ubia madhubuti ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi. SOMA: Sekta ya utalii Tanzania ‘imepaa chini ya mikono’ ya Rais Samia

Akizungumzia Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Dk. Mwinyi amebainisha kuwa eneo hilo ni la kimkakati na lina uwezo mkubwa wa uwekezaji katika maeneo ya usafirishaji, mafuta na gesi, biashara na huduma nyingine za kiuchumi.Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kukaribisha wawekezaji zaidi katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Lord Swire amesema Zanzibar ni mshirika muhimu kwa CWEIC, na kwamba taasisi hiyo ipo tayari kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uwekezaji, biashara na maendeleo ya pamoja kwa manufaa ya wananchi. CWEIC ni taasisi inayoratibu na kusimamia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *