Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, amemfuta kazi balozi wa Uingereza nchini Marekani, Peter Mandelson kutokana na uhusiano wake na Jeffrey Epstein aliyepatikana na hatia ya kuwadhalilisha kingono mabinti wadogo na alifungwa jela ambapo baadae alipatikana amekufa.
Katika taarifa yake bungeni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Stephen Doughty, amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuchapishwa wiki hii barua pepe za Mandelson alizomtumia Epstein katika miaka ya 2000, barua pepe hizo zimeonesha jinsi Peter Mandelson alivyohusika na kutoa msaada kwa mfadhili wa matendo ya kufedhehesha Epstein hata alipokuwa jela kwa makosa ya udhalilishaji wa kingono.
Waziri Doughty amesema barua pepe hizo zinaonyesha kuwa ulikuwepo uhusiano wa kina kati ya Mandelson na Epstein tofauti na kile kilichojulikana alipoteuliwa kuwa balozi na kuiwakilisha Uingereza huko mjini Washington baada ya ushindi wa chama cha Labour katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.
Mandelson aliteuliwa kuwa balozi mwezi Februari 2025
“Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo katika barua pepe alizoandika Peter Mandelson, Waziri Mkuu amenitaka nimtengue kuwa balozi nchini Marekani. Baruapepe hizo zinaonyesha undani na ukubwa wa uhusiano wake na Jeffrey Epstein. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwa Mandelson alipinga hukumu aliyopewa Epstein kwa kusema kuwa haikuwa sahihi ni jambo la kusikitisha. Sisi sote, tunawajali wahasiriwa wa uhalifu wa kutisha wa Epstein, na kwa kuzingatia hilo, Mandelson amevuliwa ubalozi mara moja.”
Balozi Peter Mandelson, ambaye alichukua wadhifa wake mwezi Februari mwaka huu baada ya kupitia mchakato wa kukaguliwa amesema anajutia uhusiano wake wa awali na Epstein na kwamba hajui chochote kuhusu matendo yake ya uhalifu.
Siku ya Jumatano, gazeti la The Sun lilichapisha barua pepe ambazo zilionyesha Mandelson akimwambia Epstein “apiganie kuachiliwa mapema” muda mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 jela. Kwenye ujumbe huo wa barua pepe
Uamuzi wa kumfukuza Mandelson umefikiwa siku moja tu baada ya Waziri Mkuu Keir Starmer kusema ana “imani” na balozi huyo aliyeiwakilisha Uingereza nchini Marekani.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Stammer kabla ya ziara ya kiserikali ya Rais wa Marekani Donald Trump nchini Uingereza wiki ijayo. Wiki iliyopita Starmer alipata pigo jingine pale naibu wake, Angela Rayner, alipotangaza kuachia ngazi kwa makosa ya kulipa kodi isiyo sahihi kwenye manunuzi ya nyumba.
Mandelson, anajulikana kwa mambo ya utata, aliwahi kujiuzulu mara mbili kutoka kwenye serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair mnamo mwaka 1998 na mwaka 2001.
Vyanzo: AP/RTRE/AFP