Akizungumza kupitia ujumbe uliorushwa kwa njia ya televisheni, afisa wa ngazi wa juu wa Hamas, Fawzi Bahroun, alisema siku ya Alhamis (Septemba 11) kwamba mashambulizi ya Israel yaliyokusudiwa kuwauwa viongozi wa kundi hilo nchini Qatar, yalifanyika kwa “ushiriki mkubwa wa Marekani.”
Hata hivyo, Ikulu ya White House ilirejelea madai yake kwamba Rais Donald Trump hakuwa amekubaliana na uamuzi wa Israel kufanya mashambulizi ya kijeshi nchini Qatar, ambayo ni mshirika muhimu wa Marekani.
Ikulu hiyo ilisema Trump hakujulishwa kabla kuhusu mashambulizi hayo na aliposikia tu, alimtaka mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, kuionya Qatar mara moja, lakini wakati huo tayari mashambulizi yalishaanza.
Bahroun alisema kilichofanywa na Israel ulikuwa “uhalifu uliokusudiwa kuua mchakato mzima wa mazungumzo” na kulihujumu jukumu la wapatanishi wa Qatar na Misri.
Hata hivyo, afisa huyo wa Hamas alisema msimamo wa kundi lake kwenye meza ya mazungumzo haujabadilika na kwamba masharti yake ya kuumaliza mzozo wa Gaza yamebakia kuwa yale yale.
Waliouawa na Israel wazikwa Doha
Mjini Doha kwenyewe, hali ya usalama iliimarishwa katika Msikiti wa Sheikh Mohammed bin Abdul Wahhab siku ya Alhamis, ambapo sala ya jeneza iliswaliwa kwa ajli ya wahanga wa mashambulizi ya siku ya Jumanne yaliyofanywa na Israel.
Mtawala wa Qatar , Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, alihudhuria sala hiyo akiwa pamoja na waombolezaji wengine waliovalia kanzu na wengine sare za kijeshi.
Maiti za wahanga hao zilizikwa baadaye kwenye makaburi ya Mesaimeer hapo hapo Doha.
Baraza la Usalama lalaani mashambulizi dhidi ya Qatar
Kwa upande wake, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitowa tamko siku ya Alhamis kuyalaani mashambulizi hayo dhidi ya Qatar lakini bila kuitaja kwa jina Israel iliyofanya mauaji hayo.
Tamko hilo lilisema tu kwamba Baraza la Usalama “linatilia mkazo umuhimu wa kutokuendeleza mzozo”, huku likielezea mshikamano wake na Qatar.
Ripoti kutoka Gaza zilisema Wapalestina 34 waliuawa siku ya Alhamis, 17 kati yao wakiwa kwenye vituo vya kukusanyia misaada vinavyosimamiwa na kile kiitwacho Wakfu wa Kibinaadamu wa Gaza (GHF), shirika linaloungwa mkono na Israel na Marekani, ambalo mashirika mengine ya kibinaadamu yanalituhumu kuwa mtego wa mauti kwa raia wenye njaa katika Ukanda huo.
Hali ya mambo kwenye Jiji la Gaza, ambako Israel inaendesha kampeni yake ya kijeshi kwa kuyaporomowa majengo inayodai yanatumiliwa na Hamas kama vituo vya mawasiliano na mashambulizi, inazidi kuwa mbaya.
Utekelezaji wa amri ya kuhama kabla ya operesheni ya jeshi la ardhini unaonekana kukwama, baada ya raia waliowahi kuondoka kuamua kurejea, wakisema hakuna palipobakia salama kwenye Ukanda huo mzima, na hivyo hakuna tafauti baina ya kuondoka na kubakia.