Katika chapisho kwenye mtandao wa X Tusk amesema kuwa wangetamani kama shambulizi hilo la droni la Urusi dhidi ya Poland lingekuwa bahati mbaya lakini haikuwa hivyo na wanafahamu hilo.
Mapema leo, naibu waziri wa ulinzi wa Poland Cezary Tomczyk pia alijibu matamshi ya Trump kuhusu shambulizi hilo la Urusi.
Tomczyk amekiambia kituo cha habari cha Polsat News nchini humo kwamba ujumbe unaopaswa kumfikia Trump ni kuwa hakuna suala la makosa katika shambulizi hilo la Urusi na kusema lilikuwa la makusudi.
Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Poland anayefanya ziara nchini Ukraine hii leo Radoslaw Sikorski, amesema usiku ambao droni 19 za Urusi zilirushwa kuingia Poland, droni 400 pamoja na makombora 40 yalivuka hadi Ukraine akisema tukio hilo halikuwa la bahati mbaya.
Wizara ya mambo ya nje ya Poland imesema kwa ombi la nchi hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo mjini New york katika mkutano utakaoanza saa tisa mchana kwa majira ya eneo hilo.
Urusi na Belarus zaanza luteka kubwa ya kijeshi
Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi, imesema luteka za kijeshi zinazofanywa na nchi hiyo kwa ushirikiano na Belarus, kwa jina Zapad 2025, zinalenga kuboresha mwingiliano kati ya vitengo vya kijeshi, haswa kati ya makamanda na maafisa wakati wanapolinda kwa pamoja dhidi ya tishio.
Kabla ya kuanza kwa luteka hizo, Poland ilifunga mpaka wake wa mashariki.
Waziri wa usalama wa ndani wa nchi hiyo Marcin Kierwinski, amesema wamefanya hivyo kwasababu ya ulinzi wa raia wao.
Uingereza yaweka vikwazo vipya vinavyohusiana na Urusi
Uingereza leo imeweka vikwazo vipya vinavyohusiana na Urusi, vinavyolenga meli zinazobeba mafuta ya Urusi, pamoja na makampuni na watu binafsi wanaosambaza vifaa vya elektroniki, kemikali na vilipuzi vinavyotumika kutengeneza silaha za Urusi.
Serikali ya nchi hiyo, imesema vikwazo hivyo, ni jibu la uchokozi wa hivi karibuni wa Urusi, ikimaanisha idadi kubwa ya mashambulizi ya droni na makombora dhidi ya Ukraine katika miezi ya hivi karibuni na ukiukwaji wa anga ya jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Polandsiku ya Jumatano.