s

Chanzo cha picha, gp

    • Author, Na Mwandishi Wetu
    • Nafasi,

Rafiki yangu mmoja aliwahi kuishi jijini Doha, Qatar kwa takribani wiki moja. Aliporejea Dar es Salaam, nilimuuliza aniambie kwa nini aliamua kutofanya kazi aliyokuwa ameitiwa.

Jibu lake sijalisahau hadi leo; “Kazi ni nzuri na watu ni wazuri. Tatizo the place has no soul”. Kwa maelezo yake, mahali pale alipaona pa baridi, palipokosa uhai na uchangamfu wa Dar es Salaam.

Huwa nakumbuka hali hii kila nikikitazama Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na ushiriki wake kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambapo tayari kimeteua mgombea urais na mgombea mwenza kwa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wagombea wa CHAUMMA, Salum Mwalimu kwa urais na mgombea mwenza wake, Devotha Minja, ni waandishi wa habari maarufu wa Tanzania. Hii ndiyo mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wana habari wawili kupata fursa hii katika chama kimoja.

Mwalimu na Devotha walikuwa sehemu ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotangaza kukihama chama hicho wakidai kutofurahishwa na mwenendo wa uongozi mpya wa chama chini ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Lissu aliingia madarakani baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali baina yake na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA kabla yake, Freeman Mbowe ambapo mwanasheria huyo machachari na Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, aliibuka mshindi.

Roho kwenye siasa za Tanzania

A

Chanzo cha picha, GP

Kwa muktadha wa siasa za Tanzania, ninapozungumzia roho ya chama cha siasa, nazungumzia jambo au nguvu ya ushawishi ya chama husika ambacho inakitofautisha na vyama vingine.

Roho hujengwa na vitu viwili – ushawishi wa mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho na pili itikadi au jambo linalowaunganisha walio chini ya bendera husika.

Historia ya takribani miaka 70 ya Tanzania inatoa mafunzo kwenye suala hili. Kwa Zanzibar, ukizungumzia ukuaji wa chama cha UMMA Party na kabla yake kile cha Hizbu, ushawishi wake ulitokana zaidi na mtu mmoja – Abdulrahman Babu.

Ukiangalia ukuaji wa chama kama cha NCCR Mageuzi kwenye miaka ya 1990 utabaini kwamba ujio wa Augustine Mrema ulikipa chama hicho ‘roho’. Roho ya Chama cha Wananchi (CUF) ilikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad, sasa marehemu.

Tofauti na vyama kama NCCR Mageuzi, TLP na CUF ambavyo vilibebwa na watu – vyama vya CCM na CHADEMA vilijengwa katika misingi ya kuvutia wafuasi kwa kuonesha mbadala.

Katika kilele cha ubora wake kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010, nyota wa CHADEMA walikuwa wanasiasa kama Zitto Kabwe, Prof. Mwesiga Baregu, Prof. Kitila Mkumbo, Mzee Philemon Ndesamburo ambao silaha yao kubwa ilikuwa kujenga hoja pasi kuwa mashuhuri kama Mrema ama Maalim Seif.

Tatizo kubwa la CHAUMMA kama chama na katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu nchini Tanzania, ni kwamba chama hakina kiongozi mmoja mwenye mvuto wala kada ya watu wa aina ya Baregu watakaokifanya kipendwe kwa hoja.

Chama ambacho hakina kiongozi mwenye mvuto wa aina ya Maalim Seif, Jakaya Kikwete wa CCM (mwaka 2005), au Mrema wa 1995 au kada ya wasomi mashuhuri wa kuitengenezea itikadi na ndoto ya nchi waitakayo, ni vigumu kupiga hatua kubwa kisiasa.

Pengine hii ndiyo sababu kila mara kumekuwa na minong’ono ya mwanasiasa mashuhuri kutajwa kujiunga na chama hicho kwa sababu ya ombwe la ‘roho’ ambalo linaonekana kutamalaki CHAUMMA.

Mwanga wa matumaini kwa CHAUMMA

S

Chanzo cha picha, GP

Kwa namna siasa za Tanzania zilivyo sasa, kuna namna tatu ambazo CHAUMMA kinaweza kujijenga na kujizatiti kama mojawapo ya vyama vikubwa vya upinzani.

Namna ya kwanza ni kujihusisha na kutengeneza ukaribu na vyama vingine. Hii ni mbinu ambayo vyama vidogo duniani huitumia. Kwa mfano, kwenye uchaguzi huu, CHAUMMA inaweza kutafuta majimbo kadhaa ya uchaguzi ambayo itaweza kuingia makubaliano na chama cha ACT Wazalendo kwa malengo kuwa wasiyanie kwa pamoja majimbo hayo.

Tanzania ni nchi kubwa kwa eneo na ACT Wazalendo na CHAUMMA vyote havina uwezo wa rasilimali watu na rasilimali fedha kupambana katika majimbo yote nchini. ACT inaweza kuchagua majimbo yake 100 na CHAUMMA ikachagua hata 20 au 40 ambayo watatumia nguvu zaidi.

Namna ya pili ni kushirikiana na chama tawala. Dunia ya sasa, kuwa na serikali iliyo na mchanganyiko wa upinzani na chama tawala ni jambo la kawaida. Kimsingi, kwa sababu ya siasa za mgawanyiko duniani, hii inaonekana kuwa ni namna njema ya kupunguza migawanyiko kwenye jamii.

CHAUMMA inaweza kuamua kushirikiana na CCM kwa makubaliano fulani kama ambavyo ANC ya Afrika Kusini inaongoza kwa kushirikiana na vyama kama DA ingawa mfumo wao wa kiutawala ni tofauti na Tanzania.

Pointi yangu hapa ni kwamba CHAUMMA wanaweza kuamua kuingia dili ya aina yoyote kisiasa na CCM ili kujihakikishia inapata viti bungeni na kubaki hai badala ya kufa.

Njia ya tatu kwa CHAUMMA ni kuendelea kufanya siasa hadi utakapofika wakati ambapo vyama vyote vya upinzani vitaamua kuweka uhasama, majigambo na ‘utoto’ pembeni ili kukabiliana na CCM.

Siasa ina mizungu mingi. Rais Felix Tshisekedi aliingia madarakani wakati chama chake kikionekana kuwa cha nne kabla ya uchaguzi. Kwa sababu za kisiasa, siasa za kikanda na kiuchumi, alijikuta akiwa Rais wa DRC kutokana na kutoelewana na tofauti nyingine kubwa miongini mwa vyama vikubwa.

Wataalamu wa siasa wanasema wiki moja na hata siku moja ni muda mrefu kwenye siasa. Tuna takribani miezi miwili ya kampeni kabla ya upigaji kura. Huo ni muda mrefu katika siasa.

Imehaririwa na Florian Kaijage

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *