Makao makuu ya serikali ya Ukraine yalichomwa moto leo Jumapili, Septemba 7, mjini Kyiv wakati wa mashambulizi ya usiku ya Urusi yaliyosababisha vifo vya watu watano, ikiwa ni pamoja na wawili katika mji mkuu.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na jeshi la wanahewa la Ukraine, Urusi imerusha zaidi ya droni na makombora 800 usiku mmoja. Hii ni mara ya kwanza kwa jengo la serikali katika mji mkuu kushambuliwa, na majengo yote yalikuwa hadi sasa yameepuka mashambulizi ya Urusi. Mwishoni mwa mwezi wa Agosti 2025, shambulio lingine kubwa dhidi ya Kyiv lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 25 na kuharibu majengo ya wajumbe wa Umoja wa Ulaya na yale ya British Council.

Kulingana na idara ya huduma za dharura, watu wasiopungua wawili wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika mji mkuu wa Ukraine Kyiv. Miongoni mwa wahasiriwa ni msichana wa mwaka mmoja. Majengo kadhaa ya makazi pia yameharibiwa. “Kwa mara ya kwanza, paa na ghorofa za juu za makao makuu ya serikali zimeharibiwa na shambulio la adui,” Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko amesema kwenye Telegram, akirusha picha za jengo lililokuwa likiteketea kwa moto, lililoko karibu na ofisi ya rais na bunge.

Katikati ya jiji, mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP ameona moshi ukipanda kutoka kwenye jengo la Baraza la Mawaziri, na helikopta zikidondosha maji juu ya paa. “Ulimwengu lazima ujibu uharibifu huu sio tu kwa maneno, lakini kwa vitendo. Lazima tuongeze shinikizo la vikwazo, hasa dhidi ya mafuta na gesi ya Urusi,” Waziri Mkuu ameomba, pia akitoa wito wa Ukraine kupewa “silaha.”

Mashambulizi chini kote

Usiku wa Jumamosi, Septemba 6, kuamkia Jumapili, Septemba 7, shambulio la Urusi limeripotiwa pia katika maeneo mengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na Dnipropetrovsk. Kulingana na gavana wa kijeshi wa jimbo hilo, Sergei Lysak, mzee wa miaka 54 ameuawa na miundombinu kuharibiwa katika shambulio ambalo pia lilihusisha ndege zisizo na rubani na makombora.

Mamlaka ya Ukraine pia imeripoti mwanamke aliyeuawa kwa mabomu ya yaiyodondoshwa kutoka angani katika jimbo la Zaporizhzhia (kusini-mashariki) Jumapili asubuhi na mtu mwingine aliuawa Jumamosi jioni katika eneo la mpakani la Sumy (kaskazini mashariki). Vikosi vya Kremlin vinachikilia jumla ya takriban 20% ya arhi ya Ukraine.

Mazungumzo yamekwama

Kwa upande wa kidiplomasia, majaribio ya upatanishi yamekwama. Mnamo Agosti 15, Donald Trump alikutana na Vladimir Putin huko Alaska, kabla ya kuwapkea Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi kadhaa wa Ulaya huko Washington. Lakini hakuna maendeleo yanayoonekana ambayo yamepatikana, na Urusi inakataa wito wa kusitisha mapigano baada ya miaka mitatu na nusu ya mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu Vita vya pili vya Dunia.

Siku ya Alhamisi, Septemba 4, nchi ishirini na sita, nyingi zikiwa za Ulaya, hata hivyo ziliahidi mjini Paris kuipatia Kyiv dhamana ya usalama ili kuzuia mashambulizi yoyote zaidi baada ya uwezekano wa kukomesha uhasama. Donald Trump, kwa upande wake, alitangaza mkutano mpya na Vladimir Putin.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *