#HABARI: Jeshi la Polisi mkoani Lindi linawashikilia askari mgambo wawili kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mali mbalimbali, zikiwemo za raia mmoja anayeishi katika Manispaa ya Lindi.
Waliokamatwa ni Karimu Athuman Omari (29), Askari Mgambo namba MG. 512421, mkazi wa mtaa wa Raha Leo, na Zawadi Swedi Mohamed (22), askari mgambo namba MG. 624773, mkazi wa Mtanda – wote wakiwa wanatumikia kazi za ulinzi katika maeneo ya Manispaa ya Lindi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na mali zinazodaiwa kuibwa kutoka kwa Anita Patel, mkazi wa eneo la Sokoine, ambapo tukio hilo lilitokea majira ya saa 4 usiku.
Watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kuhusika katika tukio hilo la wizi na kueleza kuwa walitekeleza wizi huo kutoka kwenye nyumba ya mlalamikaji, ambayo inapakana na nyumba ya mtumishi wa shirika la TANESCO, ambaye ndiye aliyekuwa akiwatumia kama walinzi wake binafsi.
Katika upekuzi uliofanywa na Polisi, mbali na kukutwa na mali za mlalamikaji Anita Patel, watuhumiwa hao pia walikutwa na mali nyingine zinazodhaniwa kuwa zimeibwa kutoka maeneo mengine tofauti.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi linatoa wito kwa wananchi wote waliopotelewa au kuibiwa mali zao kufika Kituo Kikuu cha Polisi Lindi kwa ajili ya kutambua mali zao ambazo zimeokolewa katika msako huo.
Jeshi hilo limesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote watakaobainika kuhusika na matukio ya wizi au uhalifu wa aina yoyote ile.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania #uchaguzimkuu2025