
Tarehe 1 Agosti, DRC na Rwanda zilitia saini, chini ya mwamvuli wa Marekani, taarifa ya kanuni za mfumo wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda. Mfumo huu utasimamia ushirikiano wa kiuchumi kati ya Kinshasa na Kigali, utakaosaidia makubaliano ya amani yaliyohitimishwa kati ya nchi hizo mbili huko Washington mnamo Juni 27. Wakati shirika la habari la Reuters iliripoti juu ya nakala ya rasimu ya awali siku ya Jumapili, Septemba 14, RFI iliweza kupata kopi ya waraka huo wa kurasa 17.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nakala ya rasimu iliyojadiliwa siku yasJumapili, Septemba 14, inahusu sekta tatu kuu: nishati, miundombinu, na madini.
Kuhusu nishati, miradi miwili inatawala ajenda: kukamilika kwa ufadhili wa bwawa la Ruzizi III, mradi wa kimkakati kwa eneo zima, kwa upande mmoja, na uchimbaji wa ushirika na endelevu wa gesi ya methane kutoka Ziwa Kivu kuzalisha umeme, kwa upande mwingine, mpango ambao Burundi pia inahusika.
Kipaumbele kingine ni maendeleo ya pamoja ya miundombinu ya usafirishaji kwa abiria na mizigo. Hii ni pamoja na ujenzi wa maghala, bandari, na masoko, pamoja na uhamasishaji wa uwekezaji wa kibinafsi ili kusaidia ukuaji katika eneo la Maziwa Makuu. Mhimili mmoja wa kimkakati hasa unavutia hisia: Ukanda wa Lobito, uwekezaji mkubwa zaidi wa Marekani katika usafirishaji wa madini katika kanda, ambao hadi sasa unaunganisha DRC, Zambia, na Angola, na tayari umenufaika na takriban dola bilioni 6 za uwekezaji.
Kwa Marekani, changamoto ni kuunda njia mpya za usafiri wa madini kwa kuunganisha mikoa miwili mikuu ya madini ya Kongo. Lengo? Kupunguza hatari kwa wawekezaji na kufanya uwekezaji wa madini kuwa salama na faida zaidi. Tamaa iko wazi: lengo ni kujenga sekta ya viwanda yenye hadhi ya kimataifa hapa, kuanzia mgodini hadi watumiaji wa mwisho, kwa mfano kwa kuunda kanda maalum za kiuchumi zinazovuka mipaka ili kuendeleza madini na viwanda vinavyohusiana, na miundombinu bora na ajira mpya.
Kukata uhusiano kati ya madini, migogoro na vurugu
Katika sekta ya madini, mradi huu pia na zaidi ya yote unalenga kurejesha utulivu fulani. Kwa hivyo, kampuni yoyote inayoshukiwa kufadhili makundi yenye silaha au kuchochea mivutano haitajumuishwa kwenye mfumo mpya ili kukata uhusiano kati ya madini, migogoro na vurugu.
Kwa uwazi zaidi, taratibu za sasa za kikanda zitapitiwa upya, kurekebishwa, au kubadilishwa, kwa lengo la kuzifanya ziwe za kuaminika, zenye ufanisi, na zikidhi viwango vya kimataifa. Mchakato huu utahusisha sekta ya kibinafsi, kulingana na pande zinazofanya mazungumzo.
Wakati, kwa upande wa kodi, Kinshasa na Kigali zinajizatiti kuoanisha sheria na ada zao ili kukomesha magendo na kuepuka ushindani wa kodi wenye madhara, rasimu hiyo pia inaeleza kuwa pande zote mbili zitashirikiana na Marekani na washirika wengine kupata uwekezaji na kuifanya sekta hiyo kuvutia zaidi.
Mkutano wa kila mwaka wa ngazi ya juu pia hutangazwa ili kufuatilia maendeleo, kurekebisha mwelekeo, na, ikiwa ni lazima, kuhusisha washirika wengine kama vile nchi jirani.
Kulingana na makubaliano ya Juni 27, kila kitu lazima kifanye kazi ndani ya wiki mbili.