Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo kwa njia ya video, Abbas amesema licha ya maafa makubwa kwa watu wa Gaza, shambulizi la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel halikuwa na uhalali na halikuwawakilisha wananchi wa Palestina.

Amesema “Tunayakataa matendo ya Hamas ya Oktoba 7 yaliyowalenga raia wa Israel na kuwachukuwa mateka, kwa sababu matendo kama hayo hayawawakilishi watu wa Palestina wala mapambano yao ya haki kwa ajili ya uhuru na mamlaka yao.”

Abbas, ambaye amelazimika kuhutubia kwa njia ya video kwa kuwa Marekani ilimkatalia viza ya kuingia nchini humo, amesema wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na “vita vya mauaji ya kimbari, uharibifu, njaa na uhamishaji” vinavyosababishwa na Israel.

Licha ya kwamba anatawala eneo la Ukingo wa Magharibi pekee, Abbas amesisitiza kuwa serikali yake iko tayari kubeba jukumu kamili la usalama na utawala katika maeneo hayo mara vita vitakapomalizika.

Aidha, amesema yuko tayari kushirikiana na Marekani, Saudi Arabia, Ufaransa na Umoja wa Mataifa kutekeleza mpango wa amani wa Gaza uliopitishwa Septemba 22, akisema unaweza kuleta amani ya haki na ushirikiano mpana wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *