Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango amesisitiza msimamo wa muda mrefu wa bara la Afrika wa kudai kuwa na angalau viti viwili vya kudumu vyenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa Makubaliano ya Ezulwini.

Dk Mpango ametoa sisitizo hilo alipohutubia Mkutano Mkuu wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York akihimiza pia kufanyika mageuzi ya haraka ya taasisi za kifedha za kimataifa, ikiwemo mifumo ya ukadiriaji wa deni na viwango vya mkopo, ili kutoa nafasi kubwa zaidi kwa Afrika na kufungua mitaji kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu, elimu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Makamu wa Rais wa Tanzania amesema, kaulimbiu ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa ya “Kuwa Bora Pamoja: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu” ni mwito wa kurejea katika dira ya waanzilishi wa Umoja huo. Amekemea, “vita vya kinyama,” na ukosefu wa haki unaoongezeka, akisisitiza kwamba “amani ndiyo shauku kuu ya binadamu” na lazima ifuatwe bila kuchoka kupitia mazungumzo na sheria za kimataifa.

Katika haotuba yake hiyo, Mpango amelaani pia vikwazo vya upande mmoja na kuonyesha mshikamano na nchi zilizowekewa vikwazo kama Zimbabwe na Cuba, sambamba na kurudia msimamo wa Tanzania wa kuunga mkono haki ya Wapalestina na Wasaharawi ya kujitawala.

Akihitimisha hotuba yake, Makamu wa Rais wa Tanzania amenukuu maneno ya Baba wa Taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewataka viongozi kutokaa kimya mbele ya dhulma.

Kwa mujibu wa Dk Mpango Nyerere alilaani unyonyaji wa rasilimali za Afrika unaofanywa na makampuni ya kimataifa na kukemea pia ongezeko la matumizi ya kijeshi, akilitaja kama kosa la kimaadili linaloondoa rasilimali zinazoweza kutumika katika maendeleo endelevu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *