
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair yuko kwenye majadiliano ya kuongoza mamlaka ya mpito katika Ukanda wa Ghaza, ikiwa ni sehemu ya mpango unaoungwa mkono na Marekani wa utawala utakaoendesha eneo hilo la ardhi ya Palestina baada ya kuhitimishwa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa hivi sasa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel.
Vyombo vya habari vya utawala wa kizayuni na shirika la utangazaji la Uingereza BBC viliripoti siku ya Ijumaa kwamba waziri mkuu huyo wa zamani wa Uingereza ni mtu anayezingatiwa kushika nafasi hiyo.
Blair, ambaye mwaka 2003 alishirikiana na George Bush kuzipeleka vitani Uingereza na Marekani nchini Iraq, anasemekana kuwa anafanya mazungumzo juu ya suala la kuongoza baraza hilo la utawala lililopendekezwa.
Mpango huo utaanzisha mamlaka ya mpito huko Ghaza kwa kipindi cha hadi miaka mitano, bila kuijumuisha harakati ya ukombozi wa Palestina Hamas wala Mamlaka ya Ndani inayoongozwa na Mahmoud Abbas.
Kwa mujibu wa mpango huo, mamlaka hiyo ndiyo itakayokuwa na “mamlaka makuu ya kisiasa na kisheria” juu ya Ghaza katika kipindi hicho cha mpito.
Ripoti ya duru za Israel na BBC imeendelea kubainisha kuwa, makao ya mamlaka hiyo itakuwa katika mji wa Misri wa al-Arish, ulioko karibu na mpaka wa kusini wa Ghaza, na mamlaka hiyo itafanya kazi kwa msukumo wa Umoja wa Mataifa, uungaji mkono wa mataifa ya Kiarabu na ulinzi wa vikosi vya jeshi la kimataifa.
Inasemekana kuwa, kulingana na mpango huo wa vipengele 21 unaoungwa mkono na Ikulu ya White House, kampeni ya kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu huko Ghaza haitatekelezwa tena, suala ambalo lilikuwa likipigiwa upatu katika mpango mashuhuri wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuligeuza eneo hilo la Palestina kuwa sehemu ya starehe na anasa ijulikanayo kama “Riviera ya Ghaza”.
Kwa mujibu wa mpango huo, baada ya kipindi cha mpito, udhibiti wa uongozi wa Ghaza utakabidhiwa kwa Wapalestina wenyewe.
BBC imeripoti kuwa Blair amehusika moja kwa moja katika mijadala inayohusiana na uongozaji wa mamlaka hiyo ya muda ya Ghaza…/
.