
Chanzo cha picha, Getty Images
Msimamo wa Misri kwa Israel umebadilika sana hivi karibuni, na kuzua maswali kuhusu iwapo hii inaashiria uwezekano wa kutokea kwa makabiliano ya wazi kati ya nchi hizo mbili.
Katika mkutano wa dharura wa kilele wa Mataifa ya Kiarabu na Kiislamu mjini Doha Septemba 15, uliofanyika kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya uongozi wa Hamas, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi aliitaja Israel kuwa “adui” kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani mwaka 2014.
Ongezeko hili la mvutano ambalo halijawahi kushuhudiwa, lilitokana na hatua za hivi punde za kijeshi za Israel huko Gaza na eneo hilo, ni tishio kwa mkataba wa amani uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Baadhi ya vyombo vya habari na wachambuzi wameonya kuwa kuendelea kwa hali hii kunaweza kusababisha uwezekano wa kutokea makabiliano ya kijeshi.
Siku chache baada ya matamshi hayo ya Sisi, jeshi la Israel lilitangaza kuwa zaidi ya ndege 100 zisizo na rubani, baadhi zikiwa na silaha, zimeingia Israel kutoka kwenye mpaka wa Misri; suala ambalo baadhi ya vyombo vya habari vya Kiarabu vilisema linaweza kuwa ishara ya “mashambulizi ya mapema” ya Israel dhidi ya Misri.
Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu kuitambua Israel; kufuatia ziara ya kihistoria ya Anwar Sadat nchini Israel na hotuba yake katika bunge la Knesset mnamo Novemba 1977, nchi hizo mbili zilitia saini Mkataba wa Camp David mnamo Septemba 1978 na kuanzisha makubaliano ya amani ya pande mbili mnamo 1979.
Sababu za kuwa na msimamo tofauti
Cairo, ambayo ilichagua njia ya diplomasia baada ya shambulio la Hamas Oktoba 7 dhidi ya Israel, ilichukua jukumu muhimu kama mmoja wa wapatanishi wakuu kati ya Hamas na Israel kufikia usitishaji mapigano huko Gaza.
Pia ilionyesha kujizuia katika kukabiliana na chokochoko nyingi za Israel, ikiwa ni pamoja na kulipuliwa mara kwa mara kwa kivuko cha mpaka cha Rafah na Misri, uwepo wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Philadelphia, kunyakuliwa kwa Ukanda wa Morag, na kuzingirwa kwa Rafah.
Lakini mbinu hii ilibadilika sana baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Doha, ambayo yalimfanya Sisi na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani, kutoa wito wa kuwepo kwa “Kikosi cha Jeshi” kulinda usalama wa taifa wa nchi za Kiarabu.
Vyombo vya habari vya Kiarabu vilielezea shambulio hili ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Doha wakati Israel ikivuka “mstari mpya mwekundu” katika eneo hilo, na kuzua wasiwasi na uvumi kuhusu nchi nyingine ya Kiarabu ambayo Israel inaweza kuishambulia.
Kwa nini shambulio la Gaza lilisababisha mabadiliko?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mabadiliko ya sauti ya Misri yalidhihirika zaidi baada ya jeshi la Israel kutangaza kuanza mashambulizi ya ardhini kwenye mji wa Gaza jioni ya Septemba 15 na kutoa amri ya kuwahamisha mamia kwa maelfu ya raia wa Palestina kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Operesheni hiyo ilifufua hofu ya muda mrefu ya Cairo ya uhamisho wa kulazimishwa wa Wapalestina kutoka Gaza hadi Peninsula ya Sinai, suala ambalo Misri imekuwa ikizingatia mara kwa mara kuwa “mstari mwekundu” na tishio kwa usalama wa taifa lake.
Siku chache kabla ya shambulio hili, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika mahojiano na chaneli ya Telegram ya Abu Ali Express, alisisitiza haja ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza na kuishutumu Misri kwa “kuwashikilia wakaazi wa Gaza wanaotaka kuondoka eneo la vita kinyume na matakwa yao.”
Tukio hilo pia lilijiri baada ya matamshi ya Netanyahu kuhusu maono ya “Israeli Kubwa”; katika mahojiano na mtandao wa i24 wa Israel, akisema alihisi anatekeleza “ujumbe wa kihistoria na kiroho.”
Dalili za mvutano unaoongezeka

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Misri akiitaja Israel kama “adui” katika mkutano wa Doha ilionekana kama ishara muhimu ya kuongezeka kwa mvutano na dalili ya mwisho wa subira wa Cairo na ukiukaji wa Israel.
Gazeti la mrengo wa kulia la Israel Hayom liliandika kwamba hatua hii “siyo ukosoaji tu, bali ni kuhalalisha hadharani zamu ya makabiliano ya Cairo,” na kuongeza kuwa “Cairo inakaribisha makabiliano na Israel.”
Kufuatia shambulio la Doha, Misri iliripotiwa kuwa iliionya Israel, kupitia Marekani, kwamba kuwalenga viongozi wa Hamas katika ardhi ya Misri kutakuwa na “matokeo mabaya.”
Tovuti ya Middle East Eye pia iliandika katika ripoti ya kipekee kwamba Misri ilikuwa imefahamishwa hapo awali kuhusu njama ya Israel ya kuwauwa viongozi wa Hamas mjini Cairo na ikazuia moja.
Pia kumekuwa na dalili za mvutano wa kidiplomasia katika miezi ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuahirishwa kwa uteuzi wa balozi mpya wa Misri nchini Israel na kucheleweshwa kuidhinisha hati za utambulisho za Uri Rotman, mjumbe mpya wa Israel mjini Cairo.
Uwezekano wa mapambano ya kijeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Dhihirisho muhimu zaidi la mvutano huu ni kutumwa kwa vikosi vya kijeshi vya Misri katika Peninsula ya Sinai. Machi iliyopita, maafisa wa Israeli walionya juu ya “jeshi” la Sinai, wakielezea kama ukiukaji wa mkataba wa amani wa 1979.
Ripoti ya Axios, ikinukuu vyanzo vinavyofahamu suala hilo, ilisema Netanyahu ameiomba Marekani kuishinikiza Misri kupunguza uwepo wake wa kijeshi katika Rasi ya Sinai, ambayo inajumuisha baadhi ya miundombinu ya kijeshi ambayo “inaweza kutumika kwa madhumuni ya kukera.”
Hata hivyo, Cairo inasisitiza kuwa kuwepo kwa wanajeshi huko Sinai ni “kuhakikisha usalama wa mpaka dhidi ya vitisho vyote.” Mwezi uliopita, chanzo kikuu cha kijeshi kiliiambia Middle East Eye kwamba Misri imetuma takriban wanajeshi 40,000 huko Sinai Kaskazini, “karibu mara mbili ya kiwango kilichowekwa katika makubaliano ya amani.”
Misri pia imeripotiwa kupeleka mifumo ya ulinzi wa anga ya masafa marefu ya HQ-9B iliyotengenezwa na China katika maeneo ya kimkakati huko Sinai.
Vyanzo vya habari viliiambia tovuti ya Emirati The National kwamba maelfu ya watu wa kabila la Sinai, ambao hapo awali walikuwa wamejizatiti kupambana na wanamgambo hao wenye itikadi kali, walikuwa tayari kuwaunga mkono iwapo kutatokea mzozo.
Hata hivyo, vyanzo hivyohivyo vilikazia kwamba hatua hizo zilikuwa za kuzuia na na kwamba “uwezekano wa vita kati ya Misri na Israeli bado ni mdogo.”
Ahmed Youssef, profesa wa sayansi ya siasa, anaamini kwamba “ikitokea shambulio lolote la Israeli, Misri italazimika kujilinda yenyewe.”
Kinyume chake, Ali Al-Hanafi, mjumbe wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Misri, alisema uwezekano wa kutokea mzozo wa kijeshi “unategemea upande wa Israel na ukubwa wa mielekeo na matarajio yake ya kujitanua katika eneo.”
Athari za kikanda

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuongezeka kwa mvutano kati ya Misri na Israeli kunaweza kuwa na athari kubwa za kikanda, ikiwa ni pamoja na kuunda ushirikiano mpya wa kisiasa, kijeshi na ulinzi.
Saudi Arabia na Pakistan zilitia saini makubaliano ya ulinzi mnamo Septemba 17, ambayo “uchokozi wowote dhidi ya nchi yoyote unachukuliwa kuwa uchokozi dhidi ya nchi zote mbili.”
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Khawaja Asif pia alidokeza mnamo Septemba 18 kwamba nchi zingine za Kiarabu zinaweza kujiunga na mapatano hayo.
Wakati huo huo, Misri imetuma ishara kwamba inatafuta washirika na kuunda muungano mpya.
Inafanya mazoezi yake ya kwanza ya pamoja ya jeshi la majini na Uturuki katika kipindi cha miaka 13, iliyopewa jina la “Urafiki wa Bahari,” katika eneo la mashariki la Mediterania kuanzia Septemba 22 hadi 26.
Cahed Tuz, mshauri wa zamani wa serikali ya Uturuki, alielezea zoezi hilo kuwa “ujumbe wa moja kwa moja” kwa Israeli kujibu “tishio kwa eneo lote.”
Cairo pia imeongeza juhudi za kidiplomasia kukabiliana na mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza, ikifanya mazungumzo na Saudi Arabia, Qatar na Iran, ambazo zimependekeza kuunda muungano wa kijeshi wa kikanda sawa na NATO.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi