Maelfu ya raia wa Palestina waliokimbia wakitoroka mashambulio ya Israel waendelea kurejea kaskazini mwa Mji wa Gaza kufuatia makubaliano ya usitishaji wa mapigano yalioongozwa na Marekani wiki hii.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Makubaliano hayo yameibua matumaini kwamba huenda mwafaka wa kudumu ukapatikana na kumaliza mapigano kati ya Israel-Hamas, makubaliano ambayo pia yatapelekea kuachiwa kwa mateka waliochukuliwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 2023.
Licha ya kuwepo kwa matumaini makubwa ya kupata kwa mwafaka wa kudumu, maswali bado yanaendelea kuibuliwa
kwamba ni nani atachukua uongozi wa Mji wa Gaza wakati wanajeshi wa Israel wakidaiwa kuanza kuondoka kutoka Gaza.

Changamoto nyengine ni iwapo wapiganaji wa Hamas wataweka chini silaha zao kama ilivyopendekezwa katika mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu usitishaji wa vita.
Katika hatua nyengine Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesisitiza kwamba Isreael inaweza kuanzisha tena mashambulio iwapo Hamas haitoweka chini silaha.
Mapigano ya miaka miwil kati ya Hamas na Israel yameuacha Mji wa Gaza ukiwa umeharibiwa vibaya zaidi, zaidi ya Waplestina Elfu 67 wakiwa wameuawa, upatikanaji wa chakula ukiwa ni channgamoto kubwa kwa wakazi wa Gaza.

Ijumaa ya wiki hii, chanzo kutoka shirika la kutoa misaada ya kibinadamu kilithibitisha kuwa bidhaa muhimu ikiwemo mafuta na gesi itaanza kuingia Gaza bila vikwazo kuanzia Jumamosi ya tarehe 11 ya mwezi huu.
Siku hiyo hiyo ya Ijumaa ya tarehe 10 ya mwezi huu wa Oktoba, malori yaliokuwa yamebeba misaada yalionekana yakisubiri katika upande mwengine wa kivuko cha Rafah yakiwa yanasubiri kufikisha misaada hiyo Gaza.
Mamlaka ya Israeli iliripoti kwamba malori 600 yaliobeba misaada yataruhusiwa kuingia Gaza kila siku kupitia Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yalioidhinishwa kimataifa.