
Ushiriki wa timu ya taifa ya utawala wa kizayuni wa Israel umefutwa katika mashindano ya Dunia ya Jimnastiki ya Jakarta Indonesia kulalamikia jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake ya mshikamano na watu wa Gaza, serikali ya Indonesia imefuta ushiriki wa timu ya Israel ya Jimnastiki katika Mashindano ya Dunia ya Gymnastics mjini Jakarta na kutangaza kuwa haitatoa visa ya kuingia kwa wanariadha kutoka Israel.
Wizara ya Sheria na Haki za Binadamu ya Indonesia imetoa taarifa na kutangaza kwamba, hakuna mjumbe auu mwakilishi wa michezo wa Israel atakayepewa visa ya kushiriki Mashindano ya Dunia ya Jimnastiki, ambayo yamepangwa kufanyika mjini Jakarta kuanzia Oktoba 19 hadi 25.
Kwa hatua hiyo, Indonesia imeupiga kalamu nyekundu rasmi msafara wa utawala wa Tel Aviv kwenye mashindano, ikielezea uamuzi wake kama kitendo cha “uaminifu kwa kanuni za maadili na kibinadamu.”
Akifafanua kuhusiana na uamuzi huo, Yusril Ihza Mahendra Waziri wa Sheria na Haki za Bibinadamu wa Indonesia amesema: “Indonesia inazingatia sera yake ya muda mrefu; hakuna uhusiano wowote na Israel utakaoanzishwa hadi pale utawala huo utakapolitambua taifa huru la Palestina.”
Hivi karibuni pia hatua ya mwisho ya mbio za baiskeli ilisitishwa kutokana na maandamano makubwa ya waungaji mkono wa Palestina, na wachezaji wa Israel walipigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya sataranji (chess) chini ya bendera ya Israel nchini Uhispania.
Katika miezi ya hivi karibuni, Israel imekabiliwa na mashinikizo makubwa katika nyaja mbalimbali kimataifa hata katika uga wa michezo ambapo timu za michezo za utawala huo zinakabiliwa na hali ya kutengwa na kususiwa na mataifa mengine.