
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) sambamba na kueleza kuwa usitishaji vita wa Gaza ni kushindwa kwa mipango michafu ya Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni amesema: “Serikali na mahakama za kimataifa zinapaswa kufuatilia kesi ya wahusika wa mauaji ya kimbari huko Gaza.”
Muhammad Baqir Qalibaf amesema hayo katika kikao cha wazi cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu leo asubuhi, na kueleza kuwa, “Awali ya yote, nasisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono ubunifu na hatua yoyote ya kukomesha jinai za kivita na mauaji ya kimbari huko Gaza ambayo inaungwa mkono na wananchi wa Palestina.”
Spika wa Bunge la Iran amesema, kusitishwa kwa kudumu mauaji hayo ya halaiki, kusitishwa uvamizi na kuikalia kwa mabavu Gaza, kuondoka wavamizi na kuacha kukalia kwa mabavu Gaza na kuondolea mzingiro, kufunguliwa kwa vivuko na uingiaji huru wa chakula, dawa na vitu vingine muhimu katika katika Uukanda huo ni miongoni mwa matakwa ya dharura ya wananchi wa Palestina na makundi ya muqawama, ambayo pia yanasisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Qalibaf ameongeza kuwa: Usitishaji vita Gaza ni hukumu ya kushindwa kwa mipango michafu ya waziri mkuu wa utawala huo kufidia kushindwa kukubwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa.
Aidha amesema, Netanyahu alitangaza malengo ya wazi ili kurejesha hali ya usalama iliyopotea kwa wavamizi wa ardhi za Palestina, muhimu zaidi ikiwa ni kuifutilia mbali Hamas, kuachiliwa kwa nguvu kwa mateka na kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza, lakini ameshindwa kufikia hata lengo moja kati ya malengo yake hayo.