Makundi ya Muqawama wa Palestina yanasisitiza kutekelezwa matakwa yao halali na ya wananchi wa Palestina katika makubaliano ya kusitisha mapigano.

Marwan Abdul-Aal, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya chama cha Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amesisitiza kuwa, suala la silaha za Muqawama halijazungumziwa katu kwenye meza ya mazungumzo na kwamba uendeshaji wa Ghaza lingali linabaki kuwa suala la kitaifa. Abdul-Aal ameashiria pia dhati halisi ya utawala wa Kizayuni na kuongezea kwa kusema: “tunakabiliana na adui ambaye hana muamana na anayekiuka makubaliano mara kwa mara”.

Makubaliano ya usitishaji vita yanafanyika katika mji wa Sharm el-Sheikh, Misri, na yanachukuliwa kama kielelezo cha kushindwa utawala wa Kizayuni, kwa sababu malengo ya mwanzo ya kijeshi na kisiasa uliyokuwa umetangaza utawala huo hayajafikiwa, na sasa umelazimika kurudi nyuma kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa.

Mafanikio uliyopata Muqawama wa Palestina katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni ni matokeo ya mchanganyiko wa nguvu za kijeshi, uungaji mkono wa wananchi, kugonga mwamba malengo ya adui na kubadilika milingano ya kieneo na kimataifa. Mafanikio hayo yanaweza kuonekana si katika medani ya vita pekee lakini pia katika uga wa kisiasa na wa vyombo vya habari. Licha ya kuandamwa na mashambulizi ya makombora na mabomu na kuwekewa mzingiro, Wapalestina wa Ghaza walidumisha na hata kuimarisha ngome ya uungaji mkono wa kijamii kwa Muqawama. Mhimili wa Muqawama katika eneo, ikiwa ni pamoja na Lebanon, Yemen, na Iraq, nao pia uliongeza msukumo wa kimaanawi na kisiasa kwa Palestina.

Mirengo ya Mhimili wa Muqawama katika eneo iliyounga mkono Ghazza

Utawala ghasibu wa kizayuni ndio ulioanzisha vita vya Ghaza; na kwa kufanya hivyo ulikuwa umejiwekea malengo maalumu. Kuanzia siku ya mwanzo kabisa ya vita, Wazayuni walitangaza kwamba walikuwa wamedhamiria kuiangamiza Hamas, kukomesha urushwaji wa makombora kutoka Ghaza kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, na bila shaka, kuwakomboa mateka wao kwa nguvu za kijeshi. Lakini wameshindwa malengo yao yote hayo.

Hii ni pamoja na kwamba Hamas haikuangamizwa; na utawala wa Kizayuni haukuweza kuwakomboa mateka wake kwa kutegemea nguvu za kijeshi. Viongozi wa Kizayuni, akiwemo hata waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu, wamekiri kwamba Hamas ingali iko hai na ina nguvu. Utawala wa Kizayuni sio tu umeshindwa kufikia malengo yake katika vita vya Ghaza, lakini umelazimika pia kukubali masharti yenye maslahi na Hamas katika masuala mbalimbali.

Uungaji mkono wa Wapalestina wa Ghaza kwa Muqawama

Ubunifu wa Hamas katika mwenenedo wa mazungumzo ya usitishaji vita na kwa kuzingatia ukweli kwamba Wamarekani na Wazayuni waliuhitaji Muqawama wa Palestina ili kuweza kutekeleza usitishaji vita ndicho kielelezo muhimu zaidi cha kuthibitisha ushindi waliopata wananchi na Muqawama wa Palestina. Muqawama wa Palestina umeinua hadhi ya nafasi yake katika milingano ya kikanda na kutambulika kama mdau huru na mwenye nguvu.

Kwa operesheni zake kali za mashambulio, Muqawama wa Palestina umeweza kuvunja ngano ya kulichukulia jeshi la utawala wa Kizayuni kuwa ni jeshi lisiloshindika. Licha ya kuwepo mtambo wa ulinzi wa anga wa Kuba la Chuma, Iron Dome, Muqawama wa Wapalestina uliweza kurusha mamia ya makombora hadi ndani kabisa ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel na kuusababishia hasara kubwa utawala wa kizayuni.

Muqawama wa Wapalestina umeweza hatimaye kujumuisha katika makubaliano ya kusitisha mapigano masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuachiliwa huru wafungwa, kukomeshwa mashambulizi, kufunguliwa vivuko, na kuondoka jeshi la kizayuni katika maeneo ya makazi ya watu huko Ghaza.

Nchi na taasisi nyingi za kimataifa zimeuunga mkono Muqawama na kuutambua kama mwakilishi wa watu wa Palestina. Muqawama wa Ghaza umeweza kuzipa nguvu simulizi za dhulma wanazofanyiwa wananchi wa Palestina na kusimama kwao imara kukabiliana na dhulma hizo na kuvutia uungaji mkono mkubwa wa watu duniani kwa piganio tukufu na halali la Wapalestina. Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti jinai za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni na kuhamasisha fikra na maoni ya umma dhidi ya utawala huo haramu.

Maandamano ya kuunga mkono Palestina kimataifa

Licha ya uharibifu mkubwa, mashinikizo na mwendelezo wa mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani, watu wa Ghaza waliendelea kuuunga mkono Muqawama na kudumisha moyo na ari ya istiqama.

Kwa hakika vita vya Ghaza vimeonyesha kuwa Muqawama wa Wapalestina sio tu umeboresha uwezo wake wa kijeshi na kimbinu, lakini pia umepata mafanikio makubwa katika nyanja za kisiasa, za vyombo vya habari na za kijamii. Vita hivi vilikuwa nukta ya mabadiliko muhimu sana katika historia ya mapambano ya Wapalestina, ambayo yameathiri milingano ya kikanda na kimataifa…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *