
Madrid, Hispania. Real Madrid imedhamiria kumuuza winga wao wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Junior, 25, dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwenda Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports, Vinicius anahitajika na Al-Hilal ambayo aliwahi kucheza Mbrazil Mwenzake Neymar Jr.
Waarabu hao wapo tayari kulipa zaidi ya Euro 250 milioni ili kuhakikisha inaipata saini ya staa huyu anayedaiwa hana furaha Madrid kwa sasa.
Moja ya sababu zinazotajwa zinamkosesha furaha ni kuwekwa benchi mara kwa mara na Kocha Xabi Alonso ambaye mara kadhaa alipoulizwa juu ya hilo alieleza ameamua tu.
Baadhi ya ripoti za hivi karibuni zilifichua Madrid inataka kumuuza staa huyu kwenda Saudia ili kupata pesa za kutosha zitakazoisaidia kukamilisha usajili wa Erling Haaland.
Jobe Bellingham
MANCHESTER United na Crystal Palace zinamfuatilia kiungo wa kati wa kimataifa wa England, Jobe Belligham anayeichezea Borussia Dortmund. Kwa mujibu wa gazeti la Bild Jobe ambaye ni mdogo wake Jude Bellingham ana asilimia kubwa za kurejea England mwakani na mazungumzo baina ya wawakilishi wa timu hizo na wazazi wake tayari yameshaanza. Man United inataka kukifanya kikosi chake kiwe na wachezaji nyota lakini wenye umri mdogo ili kucheza kwa muda mrefu.
Nathaniel Brown
ARSENAL, Manchester City na Real Madrid ni miongoni mwa klabu zilizo katika vita ya kuiwania saini ya beki kisiki wa Eitranch Frankfurt na timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 22, Nathaniel Brown. Licha ya uwepo wa vigogo wengi wanaohitaji huduma ya staa huyu, Frankfurt imepanga kutopokea ofa yoyote hadi itakapofika mwisho wa msimu huu. Nathaniel Brown ni miongoni mwa mastaa walioonyesha kiwango bora katika kikosi cha kwanza cha Frankfurt tangu ajiunge nacho.
Adam Wharton
CHELSEA imeongeza juhudi katika harakati zao za kumsajili kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton dirisha lijalo la majira ya baridi, lakini inakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa Manchester United ambayo pia inatamani sana kumsajili kiungo huyo, 21. Adam Wharton alihusishwa na vigogo hawa dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini ilishindikana kumpata baada ya Palace kugoma kumuuza kwa wakati huo.
Kenan Yildiz
MSHAMBULIAJI wa Juventus, Kenan Yildiz, 21, anatarajiwa kuwa na mpango wa kukataa ofa kutoka Arsenal, Chelsea na Manchester United na badala yake atasaini mkataba mpya wa muda mrefu na kuendelea kusalia Juventus. Kenan Yildiz, ambaye ameonyesha kiwango akiwa na Juventus na timu ya taifa ya Uturuki, anaonekana kuwa sehemu muhimu ya mpango wa muda mrefu wa Juventus na anaamini sana katika mipango ya timu hiyo.
PARIS Saint-Germain imeambiwa italazimika kulipa Pauni 52 milioni ili kumsajili kiungo wa AS Roma, Manu Kone, 24. PSG inapambana kuimarisha safu yao ya kiungo baada ya kuondoka kwa baadhi ya nyota msimu uliopita. Manu Kone, anaonekana kukubalika sana na kocha Luis Enrique anayeamini staa huyo atakuwa rahisi kuingia katika mifumo yake kwa sababu anaifahamu vizuri ligi ya Ufaransa.
Aleksandar Pavlovic
MANCHESTER United inamfuatilia kwa karibu kiungo wa kati wa Bayern Munich, Aleksandar Pavlovic, 21. Pavlovic, ambaye ameibuka kama mmoja ya viungo wadogo wanaofanya vizuri Bundesliga, anadaiwa kuwa tayari kupata changamoto mpya sehemu nyingine na amevutiwa na kiasi kikubwa cha pesa ambacho Man United imekiweka mezani kama ofa.
Hata hivyo, bado Bayern haijaamua ikiwa itamuuza au itaendelea kuwa naye.
Emmanuel Dennis
WATFORD inataka kumsajili mshambuliaji huru, Emmanuel Dennis ambaye aliachwa na Nottingham Forest Agosti mwaka huu baada ya mkataba wake kumalizika. West Ham pia inataka kumsajili mchezaji huyo, 27, raia wa Nigeria. Awali alichezea Watford kabla ya kujiunga na Forest na Watford inahitaji mshambuliaji mwenye uzoefu ili kuwasaidia.