
WAKATI Dodoma Jiji ikikaribia kumtambulisha, Amani Josiah, kukiongoza kikosi hicho, kwa sasa uongozi wa timu hiyo uko katika hatua za mwisho za kumpa majukumu mapya, Vincent Mashami raia wa Rwanda, ambaye hakidhi vigezo vya kusimamia benchi.
Hatua hiyo inajiri baada ya Dodoma Jiji kutozwa faini ya Sh15 milioni na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kutokana na kucheza mechi tatu msimu huu bila ya kuwa na kocha mkuu, baada ya Mashami kutokidhi vigezo vya kikanuni vya kuongoza benchi hilo la ufundi.
Timu hiyo imecheza mechi tatu za Ligi Kuu bila ya kocha mkuu, ikichapwa bao 1-0 na KMC (Septemba 17, 2025), ikatoka sare ya mabao 2-2 na TRA United zamani Tabora United (Septemba 20, 2025), kisha ikaifunga Coastal Union 2-0 (Septemba 27, 2025).
Baada ya hatua hiyo, uongozi wa timu hiyo ulikaa kikao cha siku tatu kwa lengo la kujadili suala hilo, ambapo kati ya mambo yaliyofikiwa ni kumkabidhi Josiah akiongoze kikosi hicho akiwa ndiye mkuu wa benchi la ufundi kwa msimu huu.
“Licha ya kufikia uamuzi wa kumteua Josiah, lakini Mashami hatutamuondoa katika benchi letu la ufundi kwa sababu tunahitaji kumpa majukumu mapya ambayo huko baadaye tunaweza kuyatangaza na kuyaweka wazi ni yapi,” kilisema chanzo chetu katika timu hiyo.
Taarifa zinaeleza, Mashami anaweza kupewa majukumu ya Mkurugenzi wa Ufundi kwa muda wakati akipambania kuboresha leseni yake (Refresher Course)’, kwa sababu aliyonayo ya CAF A haimruhusu kusimama akiwa kocha mkuu.
Mashami aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Rwanda, amejiunga na kikosi hicho cha Dodoma Jiji kwa mkataba wa mwaka mmoja, akitokea Police ya Rwanda, aliyodumu nayo kwa miaka mitatu na kutwaa mataji mbalimbali kikosini humo.
Kocha huyo ametwaa Kombe la Peace 2024, Super Cup 2025, na kuiwezesha timu hiyo ya Police kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupita takribani miaka 10, huku akitwaa pia ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na kikosi cha APR FC ya Rwanda.
Pia, ameiwezesha timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ kutinga hatua ya robo fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2020), huku akiwahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwamo za Isonga na Bugesera kwa vipindi tofauti.
Kwa upande wa Josiah, anajiunga na kikosi hicho baada ya awali kuzifundisha Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons, aliyoinusuru na janga la kushuka daraja msimu wa 2024-2025.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Dodoma Jiji baada ya kucheza mechi tatu, imekusanya pointi nne ikishika nafasi ya sita.