Aliyekuwa kocha Crystal Palace, Sam Allardyce, anaamini kuwa Liverpool watakuja kujutia kushindwa kumsajili beki Marc Guehi wakati wa usajili wa majira ya joto.
Guehi alikaribia kujiunga na Liverpool, lakini Crystal Palace ilishindwa kupata mchezaji wa kuziba nafasi yake, hivyo uhamisho huo ulishindikana siku ya mwisho ya usajili.
Allardyce ameeleza kwenye podikasti ya No Tippy Tappy Football, kuwa licha ya kutumia kiasi kikubwa cha pesa, Liverpool bado inaonekana kuwa na udhaifu kwenye safu yake ya ulinzi katika kipindi hiki cha msimu wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.

“Nadhani kinachotia wasiwasi kuhusu Liverpool ni kiasi kikubwa cha pesa kilichotumika kwenye kikosi. Na inaonekana mchezaji muhimu zaidi hajapatikana huyo ni Guehi kutoka Crystal Palace. Kwa sasa wanaonekana kuwa na matatizo kwenye safu ya ulinzi. Na unajua jinsi ninavyopenda ulinzi imara.” amesema.
Katika mechi 11 ilizocheza Liverpool msimu huu kwenye mashindano yote, imefanikiwa kuambulia ‘clean sheet’ mbili tu.

Kwa sasa, mabeki wa kati wanaoaminika katika kikosi cha Liverpool ni Virgil van Dijk na Ibrahima Konaté, huku Joe Gomez akiwa mchezaji wa akiba. Ryan Gravenberch pia anaweza kucheza kama beki wa kati iwapo kutahitajika.
Liverpool imetumia zaidi ya Pauni 400 milioni kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya kipindi cha majira ya joto.
Klabu hiyo imevunja rekodi ya usajili nchini England mara mbili, kwa kuwasajili Florian Wirtz kwa pauni 116 milioni na Alexander Isak kwa pauni 125 milioni.
Hata hivyo, ilishindwa kumsajili Marc Guehi ambaye alitarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi.