Mamlaka ya Elimu nchini (TEA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Serikali ya Canada zimekamilisha ujenzi na ukarabati wa maabara nne za majaribio ya kisayansi katika shule mbili za sekondari mkoani Songwe.

Ujenzi na ukarabati huo unaofanywa kwa ushirikiano wa taasisi hizo tatu ni muendelezo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa na taasisi hizo kwa lengo la kufanya mageuzi makubwa ya elimu nchini hususani kwa masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati).

Shule zilizonufaika na uwekezaji huo wa zaidi ya Shilingi Milioni 130 ni shule za sekondari Itumba na shule ya sekondari Bupigu zilizopo wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Umaliziaji ujenzi na ukarabati wa maabara hizo unafanyika kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, ambapo takribani Shilingi Milioni 132 zimetumika.

“Shule ya Sekondari Itumba imepokea ruzuku ya Shilingi Milioni 78.3 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya maabara, na Shule ya Sekondari Bupigu imepokea ruzuku ya Shilingi Milioni 54 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maabara mbili za Kemia na Fizikia.” Amesema Afisa Miradi kutoka TEA, Atugonza David

Nao wakuu wa shule hizo zilizonufaika wameishukuru TEA na washirika wake kwa kuwasaidia kukamilisha mradi hiyo inayotajwa kuchochea ukuaji wa elimu na hususani mahudhurio ya wasichana na ukuaji wa masomo ya sayansi.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na UNICEF inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni Tatu katika mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora.

Imeandaliwa na @moseskwindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *