Wakati Trent Alexander-Arnold alipoumia ghafla, ilionekana wazi huu ulikuwa wakati wa Dani Carvajal kuendelea kuonyesha ubora wake kwenye kikosi cha Real Madrid, baada ya kupona kufuatia kukaa nje kwa zaidi ya mwaka mzima kutokana na jeraha.

Hata hivyo, beki huyo mkongwe naye alipata majeraha mapya, na kuwekwa nje ya uwanja tena, hali iliyomlazimu kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso, kucheza kwa karibu wiki tatu bila kuwa na beki wa kulia wa asili.

Kwa sasa, Alexander-Arnold na Carvajal wanakaribia kurejea uwanjani, na huenda wakacheza katika mechi za hivi karibuni.

Arnold anatarajiwa kurudi katika mechi dhidi ya Juventus itakayopigwa kesho Jumatano, Oktoba 22, 2025, huku Carvajal akihusishwa na uwezekano wa kurejea kwenye mechi ya El Clasico mwishoni mwa wiki hii.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la MARCA, huenda Carvajal akawa na sintofahamu ya kucheza kwenye mechi ya El Clasico, kutokana na taarifa zake za kitabibu kuchelewa kutoka na kuwekwa hadharani kupitia benchi la ufundi la Real Madrid.

EL 01

Kwa mantiki hiyo, Alonso anaweza kuamua kuwa na tahadhari zaidi, kwa kutomchezesha kwenye mechi yenye presha kubwa kama El Clasico, ili kuhakikisha Carvajal anarudi akiwa fiti kabisa.

Kwa upande mwingine, ni habari njema kwa Alonso kwamba Trent Alexander-Arnold atakuwa tayari kucheza dhidi ya Barcelona.

Kwa kuwa mchezaji huyo raia wa England atakuwa tayari na anaweza kuanza, hakuna haja ya kumharakisha Carvajal kurudi, hasa ukizingatia atakuwa hajacheza kwa muda na bado hana kasi ya mechi kubwa kama El Clasico.

Kwa hali inavyoonekana, Carvajal anaweza kurejea rasmi wiki moja baada ya El Clasico kwenye mechi dhidi ya Valencia, ambapo presha itakuwa ndogo na mazingira yatakuwa rafiki zaidi kwa kurudi taratibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *