
Ziara ya Vance inafuatia mashambulizi na maswali yaliyoibuka kuhusiana na jinsi ya kusonga mbele na mpango huo kwa ajili ya amani ya kudumu.
Vance anakutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na anatarajiwa kuwepo kwenye eneo hilo la Mashariki ya Kati hadi Alhamisi.
Hapo jana wajumbe wa Marekani Steve witkoff na Jared Kushner walikuwa wa kwanza kufika Israel. Haya yanafanyika wakati ambapo mashirika ya kimataifa yanasema yanaongeza juhudi za utoaji misaada Gaza.
Abeer Etefa ni msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
“Kwa hiyo nafikiri tangu usitishwaji wa mapigano mnamo Oktoba 11, malori zaidi ya 530 yameingia Gaza na yanasaidia katika masuala ya kutoa na kusambaza chakula. Kufikia sasa kuna zaidi ya tani 6,700 za chakula, hicho ni chakula cha kuwatosha zaidi ya watu nusu milioni kwa wiki mbili,” alisema Etefa.
Shirika hilo vile vile linasema idadi hiyo bado ni ya chini ikilinganishwa na malori kati ya 500 na 600 yaliyokuwa yakiingia Gaza kila siku kabla vita.