Brazil. Gwiji wa soka la Brazil, Ronaldo De Lima alitimiza umri wa miaka 49 hapo Septemba 18, mwaka huu na kati ya waliomtakia heri ya kuzaliwa ni mkewe Celina Locks aliyemtaja R9 kama mtu mkarimu na mwema katika mambo mengi.

Celina, 35, alimweleza Ronaldo anampenda na kumheshimu kwa sababu amekuwa mwanga wa matumaini na kubwa zaidi kwa kuwa mwenza bora kitu ambacho ni chanzo cha furaha yake.

Hata hivyo, kabla ya ndoa hii na Celina, Ronaldo ana mfululizo wa hadithi za maisha ya mapenzi tangu akicheza Barcelona, Inter Milan, Real Madrid, AC Milan, Corinthians hadi alipostaafu.

Ronaldo, mshindi wa Ballon d’Or mara mbili (1997 na 2002), kwa sasa akiwa baba wa watoto wanne kutoka kwa wanawake watatu tunakwenda kutazama uhusiano wake na Celina pamoja ndoa zake tatu zilizovunjika. Inaonekana baada ya safari ndefu ya mapenzi yenye changamoto zilizosababishwa na umaarufu hatimaye Ronaldo amepata amani na utulivu katika ndoa yake na Celina, mrembo mwenye nyota zake.

Celina alizaliwa huko Curitiba katika Jimbo la Parana nchini Brazil. Huyo ni mwanamitindo ambaye amefanya kazi na kampuni nyingi za mitindo kwa miaka kadhaa.

Katika kazi yake, ameonekana akiwa amevalia vito vya Chopard na mavazi kutoka kwa wabunifu wakubwa kama Giorgio Armani, Chanel na Isabel Marant, huku akipamba majarida makubwa ya mitindo.

Pia ni mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa Celina Locks Beauty, kampuni ya vipodozi na bidhaa za urembo zilizotengenezwa kwa ajili ya mwanamke wa kisasa anayetaka kuacha alama popote aendapo.

Miezi ya hivi karibuni, Ronaldo ameonekana kutupia mitindo ya kuvutia katika hafla mbalimbali kuanzia Paris hadi Cannes.

Ni wazi Celina ndiye chanzo cha mabadiliko hayo ya kisasa kwenye mwonekano wake. Wakati mumewe akiwa mmoja wa wachezaji bora wa soka wa muda wote, si ajabu Celina ni shabiki mkubwa wa mchezo huo kutokana na asili yake.

“Katika nchi yangu, mpira wa miguu ni sehemu ya damu zetu, ni kitu tunachozaliwa nacho. Tumezoea kusimamisha shughuli zote wakati Brazil inacheza. Kwa hiyo nimekuwa shabiki tangu utotoni,” anasema.

Mwaka 2015, ndipo walikutana wakati huo Ronaldo akiwa na umri wa miaka 38, na Celina akiwa na miaka 25. Uhusiano wao ulikua polepole, tofauti na mahusiano ya awali ya Ronaldo yaliyokuwa na drama nyingi magazetini.

Wamekuwa wakionekana pamoja kwenye hafla za mitindo na safari za kifahari, huku Ronaldo akionekana kuwa na utulivu zaidi katika maisha yake ya sasa ikilinganishwa na hapo awali.

Celina ambaye mara nyingi huposti picha kwenye mitandao ya kijamii wakiwa pamoja, aliwahi kutajwa na Ronaldo katika mahojiano kama mtu mwenye upendo wa milele katika maisha.

Kwa mujibu wa Jarida la Vogue Arabia, wawili hao kwa mara ya kwanza walikutana kwenye sherehe ya mmoja wa marafiki zao lakini mambo yalienda polepole hadi kufikia tulipo sasa.

“Na wakati huo sikujali sana kuhusu yeye. Baadaye tulianza kuonana mara kwa mara kwenye mikusanyiko ya marafiki, ndipo kwa kujiamini aliponikaribia na kuniambia ananipenda, na kweli alimaanisha,” anasema Celina.

Mnamo Januari 2023, walichumbiana wakiwa mapumzikoni huko Karibiani (Dominican Republic).

Celina alieleza hakutarajia kuwa Ronaldo angemvisha pete ya uchumba siku hiyo. 

“Tulikuwa tumezungukwa na watu tunaowapenda na alinisomea hotuba nzuri aliyoiandaa kwa ajili yangu. Nililia sana lakini kwa machozi ya furaha,” Celina anaeleza.

Walia-mua kufunga ndoa Septemba 2023, katika kanisa lililopo Ibiza, kisiwa maarufu cha kifahari nchini Hispania. Wote wawili walivalia nguo za rangi ya krimu walipokuwa wakila kiapo cha ndoa madhabahuni.

Ronaldo, rais wa klabu ya Real Valladolid inayocheza Ligi Daraja la Pili Hispania (Segunda), alionekana akipiga picha za pamoja (selfie) na mashabiki kabla ya kuingia kanisani.

Nje ya kanisa, Msemaji wa Ronaldo aliwaambia waandishi wa habari ‘kapo’ hiyo imechagua kuoana Ibiza kwa sababu wanakipenda sana kisiwa hicho na ni mahali muhimu sana kwao.

“Pia wamepanga kufanya sherehe kubwa itakayo wakutanisha wageni 400 siku ya Ijumaa. Ni pale nyumbani kwa Ronaldo Cala Jondal, Ibiza,” anaeleza.

Katika sherehe, Bibi harusi (Celina) alivaa gauni lililotengenezwa na Armani Prive, pamoja na vito vya Tiffany & Co. na viatu vya Giorgio Armani, mavazi yaliyomfanya kuonekana wa gharama sana.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria walikuwepo ndugu, jamaa na marafiki akiwemo Julio Baptista, aliyekuwa mchezaji mwenzake Ronaldo pale Real Madrid alipocheza kwa miaka mitano.

“Leo tumezikutanisha familia zetu katika sherehe ndogo ya kidini, na hivyo kuashiria mwanzo wa wiki yenye sherehe nyingi,” wanaeleza wawili hao kupitia mitandao, ikiwa ni miaka saba tangu waanze kutoka pamoja.

Kwa Ronaldo, Mfungaji Bora wa Ulaya 1996/97 hii ilikuwa ndoa ya nne katika maisha yake akiwa tayari ametundika daruga zaidi ya miaka 10 nyuma. Je, hizo ndoa nyingine tatu ilikuwaje? Tukutane toleo lijalo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *