
Ethiopia imeanza mazungumzo na China kuhusu kubadili sehemu ya deni lake la dola bilioni 5.38 kuwa mikopo inayotumia sarafu ya yuan, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupunguza shinikizo la fedha za kigeni na kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
Kwa mujibu wa gavana wa Benki Kuu ya Ethiopia, Eyob Tekalign, mazungumzo hayo yalifanyika mwezi uliopita jijini Beijing na Benki ya Export-Import Bank of China, pamoja na Benki ya Watu wa China yakilenga urahisishaji wa malipo, biashara, na mpango wa kurekebisha deni.
Eyob alinukuliwa akisema baada ya mkutano wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) uliofanyika Ijumaa kwamba China ni mshirika muhimu sana kwa Ethiopia na hivyo kuna haka ya kurekebisha mfumo mabadilishano ya sarafu.
Hatua hii ya Ethiopia inafuata mfano wa Kenya, ambayo mapema mwezi huu ilikamilisha kubadili mikopo mitatu ya reli iliyofadhiliwa na China kutoka dola za Marekani hadi Yuan, hatua ambayo Wizara ya Fedha ya Kenya inasema itapunguza gharama za riba kwa takriban dola milioni 215 kwa mwaka. Nigeria pia ilirejesha mkataba wa mabadilishano wa yuan bilioni 15 (sawa na dola bilioni 2) na Benki ya Watu wa China mwezi Desemba mwaka jana ili kuunga mkono malipo ya biashara kati ya naira na yuan.
Mnamo Septemba, Waziri wa Fedha Ahmed Shide alitangaza kuwa Ethiopia na China zimekubaliana juu ya mfumo wa mabadilishano wa sarafu ili kuwezesha biashara kati ya Birr na Yuan, kama sehemu ya juhudi za kujenga upya uchumi na kupanua ushirikiano baada ya misukosuko ya kiuchumi ya miaka ya hivi karibuni.
Mwezi Januari 2024, Ethiopia ilijiungana rasmi na kundi la BRICS, linalojumuisha Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Misri, Ethiopia, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Indonesia. Kundi hili la kiuchumi limekuwa likihamasisha matumizi ya sarafu za ndani katika malipo ya kimataifa ili kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani, msimamo ambao Rais wa Marekani Donald Trump ameupinga vikali, akitishia kuweka ushuru wa kulipiza kisasi na vikwazo vya kiuchumi.