Tuzo ya Sakharov hutambua watu au taasisi zinazotetea uhuru wa kujieleza na haki za binadamu. Tangazo hilo limetolewa Jumatano na Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola.
Andrzej Poczobut, mwandishi wa gazeti la Poland Gazeta Wyborcza, anatumikia kifungo cha miaka minane gerezani nchini Belarus baada ya kupatikana na hatia ya “kuhatarisha usalama wa taifa.” Mwandishi huyo amekuwa akihusishwa na harakati za kutetea uhuru wa vyombo vya habari na haki za kisiasa nchini humo.
Mwenzake, Mzia Amaghlobeli, ni mwandishi maarufu kutoka Georgia ambaye alianzisha vyombo viwili huru vya habari. Alishtakiwa mwezi Agosti kwa kosa la kumzaba kofi mkuu wa polisi wakati wa maandamano ya kupinga serikali, kesi ambayo wanaharakati wa haki za binadamu wameitaja kuwa jaribio la kuzima uhuru wa vyombo vya habari. Amaghlobeli alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani.
Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, alisema ujasiri wa waandishi hao umewafanya kuwa alama ya mapambano ya uhuru na demokrasia.
“Kwa hivyo waandishi hao wawili wako gerezani kwa sasa kwa makosa ya kutungwa, ilhali walikuwa wakifanya kazi zao na kukemea ukosefu wa haki. Ujasiri wao umefanya wawe alama ya mapambano ya uhuru na demokrasia. Bunge hili linasimama nao, na wote wanaoendelea kudai uhuru,” amesema Metsola.
Tuzo ya Sakharov ilianzishwa mwaka 1988 kwa heshima ya Andrei Sakharov, mwanasayansi na mwanaharakati wa haki za binadamu wa Umoja wa Kisovieti, ambaye pia alikuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Ni tuzo ya juu zaidi ya Umoja wa Ulaya kwa utetezi wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.
Washindi wa tuzo hiyo huchaguliwa na wabunge wa Bunge la Ulaya baada ya kuteuliwa na makundi mbalimbali ya kisiasa. Kila mshindi hupokea zawadi ya euro 50,000.
Kiongozi wa upinzani wa Belarus, Sviatlana Tsikhanouskaya, amesema tuzo hiyo inatoa ujumbe thabiti kwa wafungwa wa kisiasa kwamba “hawajasahaulika, na kwamba uandishi wa habari si uhalifu.”
Miongoni mwa washindi wa zamani wa Tuzo ya Sakharov ni Nelson Mandela, Malala Yousafzai, na Denis Mukwege.
(APE, EBU)