
Afisa mmoja wa serikali ya Tunisia amesema kuwa takriban wahamiaji 40 kutoka Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara wamefariki dunia baada ya mashua yao kupinduka katika pwani ya Tunisia jana Jumatano, katika mojawapo ya ajali mbaya zaidi za meli katika eneo hilo katika mwaka huu.
Boti hiyo, iliyokuwa na takriban wahamiaji 70, ilizama karibu na mji wa pwani wa Mahdia. Vyombo vya habari vya Tunisia vimesema, watoto wachanga walikuwa miongoni mwa waathiriwa.
Kila wiki, mamlaka za Tunisia zimekuwa zikitangaza habari za kuzuiwa majaribio yasiyo ya kawaida ya uhamiaji kuelekea pwani ya Ulaya, na kuwakamata mamia ya wahamiaji kutoka Tunisia na nchi nyingine za Afrika ambao wanaelekea barani Ulaya kutokana na matatizo ya kiuchumi na kisiasa katika nchi zao.
Tukio la sasa linaangazia hatari zinazowakabili wahamiaji na mashinikizo yanayoongezeka kwa nchi za Kaskazini mwa Afrika ili kudhibiti njia zisizo za kawaida za wahamiaji.
Tangu mwanzoni mwa huu wa 2025, takriban watu 56,000 wamewasili katika ufuo wa Italia, likiwa ni ongezeko la 2% mwaka hadi mwaka, huku wengi wao (49,792) wakitoka Libya na waliosalia (3,947) kutoka Tunisia.