
Mshambuliji wa Liverpool Mohamed Salah na beki wa Paris Saint-Germain Achraf Hakimi ni miongoni mwa nyota 10 walioteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika wa 2025, waandaaji wa tuzo hiyo shirikisho la soka Afrika CAF limetangaza hii leo.
Salah alimaliza wa nne na Hakimi wa sita katika tuzo ya mchezaji bora wa dunia ya Ballon d’Or ya 2025. Salah amewahi kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka mara mbili huku nahodha wa Morocco, Hakimi akiitafuta tuzo hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika orodha hiyo ni wachezaji wawili tu ambao wanacheza katika ligi ya ndani ya bara la Afrika, wachezaji hao ni raia wa Kongo, Fiston Mayele kutoka klabu ya Pyramids FC ya Misri na Oussama Lamlioui anayechezea RS Berkane ya Morocco.
Mshindi wa mara ya mwisho wa tuzo hiyo Mnigeria Ademola Lookman, hayupo kwenye orodha hiyo.