Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Hakim Ziyech amefikia makubaliano ya kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Mwandishi nguli wa Habari za usajili, Fabrizio Romano, Ziyech amejiunga na Wydad akiwa mchezaji huru kwani hakuwa na timu tangu alipoachana na Al-Duhail ya Qatar baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

Ndani ya Wydad, Ziyech atacheza sambamba na kiungo wa zamani wa Yanga, Stephane Aziz Ki.

Maisha ya kisoka kwa Ziyech mwenye umri wa miaka 32 yalianza kuwa magumu kuanzia Januari 2023 pale aliposhindwa kukamilisha uhamisho wa mkopo wa kujiunga na PSG ya Ufaransa ambayo ilikuwa inamuwania.

Uhamisho huo ulikwama kutokana na uongozi wa Chelsea kuchelewesha baadhi ya nyaraka jambo lililofanya hadi dirisha lilipofungwa uhamisho huo kushindwa kukamilika.

Baada ya msimu wa 2022/2023 kumalizika, mshambuliaji huyo Agosti, 2023 alikamilisha uhamisho wa mkopo kwa msimu mzima akijiunga na Galatasaray ya Uturuki.

Galatasaray ilivutiwa naye na kumpa mkataba ambao aliutumikia hadi Januari 29, 2023 alipofikia makubaliano na klabu hiyo kuuvunja.

Baada ya hapo alijiunga na Al Duhail kwa mkataba wa muda mfupi ambao ulifikia tamati katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi na kuanzia hapo, hakupata timu nyingine hadi alipojiunga na Wydad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *