Liverpool imekomesha mwenendo wao mbaya wa kupoteza mechi kwa kishindo, baada ya kutoka nyuma na kuicharaza Eintracht Frankfurt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Oktoba 22, 2025.
Baada ya kuanza msimu kwa kasi kwa kushinda mechi saba mfululizo katika michuano yote, Liverpool ilipoteza mwelekeo kwa kufungwa mechi nne mfululizo, ikiwemo dhidi ya mahasimu wao Manchester United kwenye Ligi Kuu siku ya Jumapili.
Awali, ilionekana kama hali hiyo mbaya ingeendelea baada ya kufanya mwanzo wa kusuasua nchini Ujerumani na kuruhusu bao la kuongoza lililofungwa na beki wa zamani wa Leeds, Rasmus Kristensen.
Hata hivyo, Liverpool waligeuza matokeo baada ya Ekitike aliyekuwa akianza kwa mara ya kwanza pamoja na mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka la Uingereza, Alexander Isak kusawazisha dakika 10 kabla ya mapumziko kwa kukimbia kwa ustadi akipokea pasi nzuri ya Andy Robertson na kumalizia kwa utulivu mkubwa.
Virgil van Dijk aliongeza bao la pili dakika nne baadaye kwa kichwa kizuri kutoka kona, kabla ya Ibrahima Konaté kufanya matokeo kuwa 3-1 dakika moja kabla ya kipindi cha kwanza kuisha baada ya naye kufunga kwa kichwa kupitia kona.
Ushirikiano wa Ekitike na Isak ulidumu kwa dakika 45 pekee, kwani aliyekuwa mshambuliaji wa Newcastle hakurudi kipindi cha pili.
Wakati huo Liverpool tayari ilikuwa imeshavunja nguvu za wapinzani wao, lakini iliendelea kutafuta ushindi wa kishindo kwa kuongeza mabao mawili zaidi katika kipindi cha pili ambacho ilikitawala kikamilifu.
Cody Gakpo alifunga bao lake la nne msimu huu kwa kumalizia pasi ya Florian Wirtz, kabla ya Dominik Szoboszlai kufunga shuti kali la mbali lililokamilisha ushindi huo mnono, mechi ikichezwa Deutsche Bank Park, Ujerumani.
Salah mambo magumu
Salah alianza mechi hiyo akiwa benchi, huku kocha Arne Slot akimpa nafasi dakika ya 74 wakati Liverpool ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 5-1.
Dakika za mwisho za mchezo, Salah alipata nafasi nzuri ya kumpasia Wirtz ambaye bado hajafunga tangu ajiunge na Liverpool kwa dau nono la pauni milioni 116 akitokea Bayer Leverkusen, lakini badala yake akaamua kupiga mwenyewe jambo lililowakera mashabiki.
Salah alikuwa kwenye kiwango cha juu msimu uliopita, akifunga magoli 34 na kutoa pasi 23 za mabao katika michezo 52, na hata kutunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA, lakini safari hii mambo si mazuri amefunga magoli matatu pekee na kutoa asisti tatu kwenye mechi 12 za msimu huu.