Alassane Ouattara anagombea tena akiwa na chama tawala cha Rassemblement des Houphouetistes pour la Paix chenye kaulimbiu “Kwa ajili ya Taifa Kubwa.”
Watu milioni 8.7 wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huo, unaokutanisha pia vyama vinne dhaifu vya upinzani vitakavyopambana na Ouattara.
Maelfu ya wafuasi wa Ouattara wamekusanyika Ijumaa katikati mwa mji wa Abidjan baada ya kusherehekea mitaani jana Alhamisi, ambapo Ouattara alikuwa akihitimisha kampeni zake.
“Tumeiimarisha Ivory Coast. Taifa hili limeshuhudia ukuaji usio wa kawaida tangu mwaka 2011 na ni lazima liendelee hivi. Ni lazima liendelee kwa angalau miaka mitano ijayo ili kutupa fursa ya kuboresha pale tuliposhindwa,” alisikika Ouattara.
Wagombea wa upinzani hawana nafasi kubwa
Wagombea wengine pia walielezea sera zao kwa mara ya mwishomwisho mbele ya wafuasi wao. Mke wa rais wa zamani Simone Gbagbo alifanya mkutano wake wa mwisho katika eneo la Aboisso, mashariki mwa nchi hiyo huku Waziri wa zamani wa Biashara Jean-Louis Billon naye akifanya kampeni zake za mwisho huko Bouake, katikati mwa nchi
Wachambuzi wanasema wagombea hao hawana nafasi yoyote na hasa kwa kuwa wapinzani wawili wakubwa, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Credit SuisseTidjane Thiam wa chama cha PDCI pamoja na rais wa zamani Laurent Gbagbo wa chama cha PPA-CI wakiwa wameenguliwa kwenye uchaguzi.
Siku ya Jumatano, Gbagbo ambaye sasa ni mpinzani aliitaja kura hiyo kama “mapinduzi ya kiraia” huku akielezea kuwaunga mkono wale wanaopinga wizi wa kura. Amesema hayo kwenye mahojiano na chombo cha habari cha AFO na kwa pamoja, wawili hao wametoa wito wa maandamano ambayo yamezuiwa na serikali, wakisema yatasababisha vurugu kwa umma.
Vikosi vya usalama vyamwagwa mitaani
Vikosi vya usalama vipatavyo 44,000 vimemwagwa kote nchini humo, tayari kuyadhibiti maandamano ikiwa yatafanyika na hasa kwenye maeneo ya upinzani yaliyoko kusini na magharibi mwa nchi.
Shughuli kwenye mji huo mkuu zimezorota kwa kuwa maduka kwenye maeneo mengi yamefungwa kutokana na hofu ya kuzuka kwa machafuko.
Mitaa ya Abidjan imetawaliwa na mabango yenye picha za Ouattara, huku mabango ya wapinzani wake yakiwa ni machache mno, hii ikichukuliwa kama ishara ya rais huyo kushinda tena kwenye uchaguzi wa kesho.
Uchaguzi huo wa rais wa Oktoba 25 kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi, unafanyika baada ya muongo mmoja wa utulivu kiasi kufuatia mgogoro wa baada ya uchaguzi wa 2010–2011 uliosababisha vifo vya maelfu ya watu na taifa kugawanyika. Licha ya hayo, taifa hilo linalotambulika rasmi kama Cote d’ Ivoire, tangu wakati huo limekuwa na ukuaji mzuri uchumi, ingawa mivutano ya kisiasa bado ingalipo.